Habari za Kitaifa

Hatari kwa Gachagua hamahama zikitawala mrengo wake Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI May 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua ameanza kukabiliwa na maasi Mlima Kenya baada ya baadhi ya wandani wake kumtoroka, wa hivi punde kufanya hivyo akiwa aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu.

Kabla ya Bw Wambugu, waliokuwa wandani wake Mary wa Maua (Mbunge wa Maragua) na Peter Kihungi (Kangema) nao waligura kambi yake. Wengine ambao walikuwa wakimuunga Bw Gachagua na wamerudi kwenye kambi ya Rais William Ruto ni wabunge Karemba Muchangi (Runyenjes), Wainaina Chieni (Kieni) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Embu Njoki Njeru.

Wengine ambao wamekimya na ni vigumu kubaini iwapo bado wapo kwa Bw Gachagua ni Mbunge wa Kandara Chege Njuguna na mwenzake wa Githunguri Gathoni wa Muchomba.

Wawili hao licha ya kuwa walikuwa wafuasi sugu wa Bw Gachagua, hawakujitokeza nyumbani kwake Wamunyoro Jumapili wiki ya juzi.  Bw Gachagua alikuwa mwenyeji wa vinara wengine wa upinzani wakimewo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa DAP Kenya Eugene Wamalwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí.

Badala ya kuhudhuria mkutano huo Bi Wamuchomba alikuwa mji wa Kenol, nyumbani kwake ambako alikutana na vijana kisha akachapisha ujumbe kwenye ukurasa wake wa Facebook ambao unaweza kufasiriwa kuwa ameamua kuchukua mkondo mwingine wa kisiasa.

Kabla ya kupoteza tapo hili la wanasiasa, aliyekuwa naibu rais alikuwa amewapoteza mbunge wa Mathira Eric Wamumbi na mkewe Betty Maina ambaye ni mbunge mwakilishi wa kike wa Murangá.

Itakumbukwa kuwa ni Bw Gachagua alichukua jukumu la mzazi na kuandamana na  Bw Wamumbi kumlipia Bi Maina mahari na kuomba wakwe zake wampe mke.

Kinaya ni kuwa baada ya kukosana, Bw Wamumbi na Bi Maina walikuwa mstari wa mbele kuunga mkono hoja ya kumtimua Bw Gachagua kama naibu rais mnamo Oktoba mwaka jana.

Bi Wa Maua aligura kambi ya Bw Gachagua ambaye alikuwa mbunge wa Mathira kati ya 2017-2022, mnamo Aprili 3, 2025 wakati wa ziara ya siku sita ya Rais Ruto Mlima Kenya.

“Kuondolewa kwa Gachagua kulikuwa ni utelezi tu. Lazima nikiri kwamba nimekuwa nikiongea na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki tangu Novemba na Rais tangu Disemba mwaka jana,” akasema Bi Wa Maua wakati huo akitangaza ametalikiana na Bw Gachagua.

Mbunge huyo aliongeza kuwa hasira kutokana na kutimuliwa kwa Bw Gachagua zilikuwa zimepoa na sasa kazi yake ni kuhakikisha wakazi wa eneobunge lake wanapokea miradi ya maendeleo.

Kuondoka kwa Bw Ngunjiri kuliwashangaza wengi ikizingatiwa amekuwa naye na hata alipinga vikali kutimuliwa kwake. Bw Ngunjiri alirejea Jubilee na kutangaza kuwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ndiye kigogo wa siasa za Mlima Kenya na hata akasema Rais Ruto ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa kwa muhula wa pili.

“Watu wanaendelea kupona kutokana na kutimuliwa kwa Gachagua na sasa hata viongozi waliombandua wanasikizwa. Sasa nimerejea kwenye siasa kwa sababu kazi yangu wakati huo ilikuwa kumjenga kimawasiliano,” akasema Bw Ngunjiri akilalamika hisani yake imelipizwa kwa matusi na mrengo wa aliyekuwa naibu rais.

Bw Kihungi naye alihama mnamo Februari na akamtembelea Rais ikuluni. Alijitetea akisema ni ngumu kupigana dhidi ya serikali na kutimiza miradi ya maendeleo.

“Ni ngumu kuhudumu huku ukipigana na serikali. Nawaomba Rais na Gachagua waridhiane ili iwe rahisi kufanyia raia kazi Mlima Kenya,” akasema.

Jumapili, Bw Gachagua alitangaza vita dhidi ya wale ambao alidai wamewasaliti wakazi wa Mlima Kenya kwa kufanya kazi na Rais Ruto akiahidi kumfanya awe rais wa muhula moja.

Tafsiri na Cecil Odongo