Habari za Kitaifa

Hatujuti kamwe kuunga Ruto, Jumwa na Namwamba wasisitiza

Na BENSON MATHEKA October 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WALIOKUWA Mawaziri, Bi Aisha Jumwa na Ababu Namwamba wamesisitiza kuwa hawajuti kumuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu uliopita licha ya kukosa kurejeshwa katika Baraza la Mawaziri.

Bi Jumwa na Bw Namwamba walikanusha ripoti kwamba ni miongoni mwa wanasiasa wanaolalamika kwa kutorudishwa kazini au kuteuliwa katika nyadhifa serikalini.

“Hakuna siku hata moja nitawahi kujuta kumuunga mkono Rais William Ruto. Ni kiongozi ninayemuamini na atakayesongesha Kenya mbele. Muache siasa duni. Mimi nitasimama na Rais Ruto mpaka mwisho,” alisema kupitia akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii akijibu ripoti kwamba ni mmoja wa wanaolalamika kwa kukosa nyadhifa serikalini.

“Eti baridi yatupiga, baridi gani?” alishangaa Bi Jumwa ambaye ni mmoja wa wanasiasa waanzilishi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) waliokuwa msitari wa mbele kumpigia debe Rais Ruto na mwanachama wa Baraza la Kwanza la Mawaziri la Serikali ya Kenya Kwanza. Bw Namwamba alisema hajawahi kulalamika kwa kufutwa uwaziri.

“Mimi Ababu Terrah ni Rock (Mwamba) nipigwe na baridi kweli,” alisema kupitia akaunti zake za kijamii.

Rais Ruto alipovunja baraza lake la mawaziri mnamo Julai mwaka huu, aliwaacha nje mawaziri kadhaa wakiwemo Bi Jumwa na Bw Namwamba.

Rais aliwahakikishia wakazi wa Kilifi na Pwani kwa jumula kwamba hawezi kumsahau mbunge huyo wa zamani wa Malindi ambaye alisimama naye wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Alipokosa kurejeshwa kazini, baadhi ya wanachama wa UDA Kilifi, walihisi Rais Ruto alienda kinyume na matarajio yao ya Bi Jumwa kujumuishwa kikamilifu kwenye nafasi kuu za uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza licha ya kuwa mstari wa mbele kupeperusha bendera ya kaunti hiyo.

Mshirikishi wa chama cha UDA katika Kaunti hiyo, Bw Moses Matano, alisema huenda uchaguzi wa viongozi wa UDA ambao ulikuwa ufanyike Kaunti hiyo haungefanyika baada ya Bi Jumwa kukosa kuteuliwa katika baraza la mawaziri.

“Tumeshangazwa sana kwa sababu zile shida Aisha amepitia ndani ya Kilifi Kaunti ni shida ambazo mtu yeyote mwenye roho nyepesi angeacha ushirika wake na Rais Ruto, lakini Bi Jumwa alisimama naye kidete na kuhakikisha anazoa kura za Kilifi kwa kueneza ajenda ya UDA,” alisema Bw Matano.

Mchanganuzi wa siasa Kaunti ya Kilifi, Bw Frankiline Ndoro, alitaja hatua hiyo kama njama tu ya Rais Ruto kumeza ODM na kujizolea kura alizokosa katika uchaguzi uliopita.

“Kama hakuna Bi Jumwa hakuna UDA huku Kilifi na tutaunda chama kingine maana tumekosa mwelekeo,” alisema Bw Ndoro.

Hata hivyo, Bi Jumwa alisema hakuhitaji kupigiwa debe, kufanyiwa kampeni wala kutetewa na wanasiasa ili ateuliwe tena kwenye baraza la mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza.

“Sihitaji kutetewa wala kupigiwa debe ili niteuliwe tena kwenye baraza la mawaziri, Rais ananijua na akiona vyema kunirejesha kazini nitashukuru na pia akiniambia nipumzike bado nitamshukuru,” alisema Bi Jumwa.

“Msinipigie debe, Rais ananijua,” Bi Jumwa alisema wakati huo.