Hawarushi mawe, hawavunji maduka: Vijana waleta mwamko mpya wa mapambano
VIJANA wa Kizazi kipya almaarufu Gen Z na Millennials, waliandaa maandamano ya aina yake Nairobi, Jumanne, Juni 18, 2024, kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Maandamano hayo yalikuwa tofauti na ya miaka 10 iliyopita hapa nchini, kwa kukosa kufanya vurugu. Kizazi hicho kipya kiliandamana bila ya wanasiasa kuwepo. Walitaka serikali kutupa mswada huo ambao ulisheheni ushuru kwenye sodo, mkate, magari, mafuta ya kupika na kutuma pesa kwa simu.
Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali, Mwazilishi wa Kituo cha Haki za Kijamii cha Mathare, Bi Wanjira Wanjiru, alisema kuwa maandamano yanayoendelea kote nchini yakiongozwa na vijana ni ya kukomboa nchi kutoka kwa uongozi mbaya.
“Jumanne ilikuwa siku nzuri sana kwa vijana kukomboa nchi,” alisimulia Bi Wanjiru.
Alisisitiza mwamko huo mpya utaendelea hadi wakati viongozi waliochangulia wanawakilisha vijana ifaavyo. Alighadhabishwa na wabunge ambao wanaunga mswada huo.
“Wabunge wetu wametuangusha sana. Iweje, hoja za ushuru zinatolewa pale bila kupinga? Tumesoma Mswada huo na kuona kuwa sisi vijana ambao ni asilimia kubwa ya wapiga kura tunaumizwa,” alisema Bi Wanjiru.
Mbona maandamano hayo yakafanyika kwa masaa mengi?
Bi Wanjiru ambaye anapigania haki za binadamu, alisema walitathmini hali ya usalama na kuwa na ukakamavu wa kufanya maandamano.
“Unapoingia kwenye maandamano lazima utumie zile hisia tano ambazo Mungu alikupa. Pia tathmini hali ya usalama ilivyo. Usiende tuu maana wengine wanafanya hivyo, hapana. Kisha hakikisha upo kwenye kundi fulani,” aliongeza Bi Wanjiru.
Bi Wanjiru alionya baadahi ya maafisa ambao hufuata maagizo ya wakuu wao bila kujali pia wao ni Wakenya wa kawaida. Alieleza serikali kuwa ni makosa kuwatia nguvuni vijana ambao hawana hatia.
“Si mara ya kwanza kukamatwa na polisi maana huwa najua sijakosea. Mbona niwe na uwoga, hatufai kuwapa polisi nafasi ya sisi kuonekana waoga. Maandamano tunayofanya nchini ni kulingana na katiba.”
Bi Wanjiru alisema licha ya kulelewa kwenye vitongoji kuna msisimko wa vijana ambao wana nia ya kubadilisha taifa. Hata hivyo, alikema Mbunge wa Mbeere Kaskazini Bw Geoffrey Ruku aliyewasilisha mswada bungeni wa kuwafunga jela waandamanaji kwa mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh100,000.
“Naona kuna mbunge ambaye amewasilisha mswada kuwa tunahitaji kuwa na kibali cha kufanya maandamano, hao ndio viongozi tunafaa kuwaondoa kwenye mamlaka.”