Habari za Kitaifa

Hisia za Mlima Kenya kufuatia kufutwa kazi kwa Muturi

Na GITONGA MARETE NA GEORGE MUNENE March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUTIMULIWA kwa Waziri wa Huduma za Umma, Justin Muturi, kumepokelewa kwa hisia mseto eneo la Mlima Kenya, baadhi ya viongozi wakisema kulichelewa sana, huku wengine wakisema ni hatua ya serikali ya Rais William Ruto kuendelea kutenga eneo hilo.

Rais Ruto alimfuta kazi Muturi Jumatano, Machi 26, 2025 na kumteua Mbunge wa Mbeere Kaskazini, Geoffrey Ruku, ambaye anatoka katika eneo hilo na pia mwanachama wa Democratic Party (DP), chama cha Bw Muturi.

Mbunge wa Nyeri Mjini, Duncan Mathenge alisema Bw Muturi “aliomba kufutwa kazi na alijua angefutwa,” akiongeza kuwa hatua hiyo haikuwashangaza viongozi wa eneo hilo.

Alisema kuwa Bw Muturi alikiuka kanuni ya uwajibikaji wa pamoja inayowafunga Mawaziri wote, na hivyo, kuendelea kwake kushiriki katika maamuzi ya kitaifa hakukuwa na maana.

“Alikuwa na nafasi ya kukaa katika chombo hiki muhimu kinachofanya maamuzi kwa nchi na alikuwa na fursa ya kubadilisha kile alichohisi hakikuwa sawa. Lakini aliamua kukosoa serikali kutoka ndani, hivyo ilikuwa lazima aondolewe,” Bw Mathenge aliambia Taifa Leo katika mahojiano kwa njia ya simu.

Mbunge huyo alisema kuwa kukataa kwa Bw Muturi kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri na kutoa masharti kwa Rais kuwa angehudhuria tu iwapo masuala ya utekaji nyara na mauaji ya kiholela yangeshughulikiwa, kulikuwa na nia mbaya.

“Alianza kupiga kelele na kuzungumzia masuala haya katika vyombo vya habari, jambo lililovuruga mshikamano wa taasisi hii muhimu ya serikali, hivyo akakiuka kanuni,” alisema Bw Mathenge, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Ruto.

Mwenyekiti wa Jubilee Kaunti ya Kirinyaga, Mureithi Kang’ara, aliunga mkono mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri, akisema Rais ana haki ya kuteua watu wanaotaka kufanya kazi naye.

“Hakuna njia ambayo Rais anaweza kuhifadhi Mawaziri wanaompinga kila mara. Hata nyumbani, hauwezi kuishi na mke ambaye hakuheshimu,” alisema Bw Kang’ara.

Hata hivyo, wandani wa Naibu Rais wa zamani, Rigathi Gachagua, walisema kuwa kutimuliwa kwa Bw Muturi ni jaribio la kuendelea kutenga eneo la Mlima Kenya kutoka siasa za kitaifa.

Mbunge wa Tetu, Geoffrey Wandeto, alisema: “Huku ni kuendelea kutenga viongozi wa Mlima Kenya wanaosema ukweli wao.

Tumeona kilichotokea bungeni pale wandani wa naibu rais wa zamani walipotimuliwa kutoka kamati mbalimbali. Eneo la Mlima Kenya linatengwa kabisa,” alisema Bw Wandeto.

Aliongeza: “Bw Muturi alifutwa kazi kwa kudai kuwa serikali ishughulikie yale yale yanayowaumiza Wakenya. Uteuzi wa Bw Ruku ni hila kwa sababu anatoka eneo moja na Bw Muturi, lakini hii haitabadili mtazamo wa watu wa eneo hili kuhusu serikali hii. Watu wanajihisi wametengwa na kudanganywa na serikali waliyoipigia kura kwa wingi,” alisema.

Baadhi ya wakazi wa Embu walipongeza hatua hiyo huku wengine wakisema Rais alikosea kumfuta kazi Bw Muturi.