Habari za Kitaifa

Hofu magenge na majangili wakitawala, polisi wakisemekana kuwakodisha bunduki 

Na WAANDISHI WETU April 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KENYA inakumbwa na wimbi jipya la uhalifu unaoendeshwa na magenge hatari ya vijana na majangili wanaotishia usalama wa wananchi, mali zao, na hata maafisa wa usalama.

Kutoka Meru ambako mashambulizi ya majangili wanaua maafisa wa polisi na kuiba mifugo, Pwani na hadi sehemu za Magharibi kama Bumala, wakazi wanahangaishwa na magenge ya vijana ambayo yamekuwa kero kwa wakazi.

Magenge yamekuwa na ujasiri wa ajabu kiasi cha kuweka vizuizi vya barabarani katika baadhi ya maeneo kuvizia na kuibia watu.

Katika Kaunti ya Meru, tukio la hivi karibuni la mauaji ya maafisa watatu wa Polisi wa Akiba (NPR) limezua hasira na vilio vya wanasiasa na wananchi kwa jumla.

Takriban majangili 30 walivamia eneo la Mea na kutwaa silaha tatu na risasi 180.

Shambulizi lilitokea karibu na kituo cha polisi, jambo linaloonyesha ujasiri wa hali ya juu wa wahalifu hao.

Mbunge wa Buuri, Bw Mugambi Rindikiri, alikashifu vikali serikali kwa kutochukua hatua madhubuti kuhakikishia wakazi usalama.

“Waziri wa Usalama wa Ndani amekuwa akifurahia ofisi ya kifahari Nairobi huku watu wetu wakichinjwa. Hatutaki tena mikutano ya bodi ya usalama, tunataka hatua halisi zichukuliwe,” alisema Rindikiri kwa hasira.

Wabunge wenzake akiwemo Julius Taitumu wa Igembe North na Dan Kiili wa Igembe Central walimuunga mkono wakitaka fidia kwa wafugaji waliopoteza mifugo.

“Hii sio siasa. Rais anapaswa kujua waliopewa usukani wa usalama wamefeli. Waziri Murkomen asimame kidete au ajiondoe,” alisema Mbunge Mpuru Aburi.

Waziri Murkomen alitembelea Meru mwaka jana, 2024, na kutangaza kuwa serikali itaanzisha operesheni ya pamoja na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusaka majangili wanaojificha kwenye msitu wa Mukogondo.

“Tumekubaliana na makamanda wa usalama kutoka ukanda huu na tumeanzisha kambi ya operesheni Kirimon, Laikipia. KDF itaongoza juhudi za kusaka majangili waliogeuza msitu huo kuwa maficho yao,” alisema Murkomen akiwa Meru.

Baadhi ya sehemu ambazo ni makao ya majangili ni Kaunti za Samburu, Baringo, Turkana, Pokot Magharibi, Isiolo, Laikipia, Marsabit na hivi punde mashambulizi yamechacha Meru.

Huku Meru ikilia kwa kuhangaishwa na majangili, Pwani na maeneo mengine kama Busia yanapambana na magenge ya vijana yanayoibuka kila uchao.

Miongoni mwao ni Mapangale, genge hatari linaloendesha uhalifu wa kutumia silaha na mapanga huku polisi wakionekana kulegea.

Katika Bumala, Busia, tukio la mauaji ya mwanabodaboda, Vincent Barasa, ambaye alifyatuliwa risasi nje ya duka lililovamiwa, limezua hisia kali.

Genge hilo liliiba zaidi ya Sh 600, 000 na kutoroka kwa pikipiki tatu.

Wakazi walielezea kusikitishwa na polisi waliofika saa nne baada ya tukio, licha ya kituo cha polisi kuwa mita 300 tu kutoka eneo la tukio.

“Tuliwapigia simu polisi na hata OCS, lakini walichelewa mno. Polisi walipofika, walikamata raia ovyo na hata kumpiga risasi mtu mwingine karibu na kituo cha mafuta,” alisema Nicholas Onyango, mkazi wa Bumala.

Wananchi wanalalamikia wizi na mashambulizi usiku huku wakitaja maeneo maarufu kama Masebula, Nyamanga, Bujumba, Kwa Tangi na Chuma Mbili kama maeneo ambayo yamekuwa maarufu kwa magenge.

“Wezi wamegeuza maeneo haya kuwa ‘vizuizi vya barabarani’ na watu wengi wanakwepa kupita kwenye maeneo haya hatari, badala yake wanachagua njia ndefu kufika nyumbani salama,” alisema Bw Isaiah Magome, mwenyekiti wa usalama wa wanabodaboda, Bumala.

Baadhi ya wakazi wanadai baadhi ya maafisa wa polisi wanashirikiana na wahalifu, hata kufikia hatua ya kukodisha silaha.

Wanaitaka serikali kuhamisha maafisa wote wa kituo cha polisi cha Bumala na kuleta wengine wapya.

Kamishna wa Kaunti ya Busia, Mwachaunga Chaunga, alithibitisha kuwa maafisa wawili wa polisi walikamatwa kwa kuhusika na tukio la kupiga risasi mwananchi kwenye baa.

Aliahidi kuimarisha usalama kwa kuongeza maafisa kutoka maeneo mengine.

Mapangale si genge pekee linalohangaisha wananchi. Katika historia ya Kenya, magenge kama Mungiki, Chinkororo, na 24 Brothers Gang yamekuwa mfano wa jinsi makundi haya yanavyoibuka katika jami kutoka vijijini hadi miji mikuu.

Kila genge lina mfumo wake, lakini lengo ni moja: kuvuruga amani, kueneza hofu, na kupata faida kupitia uhalifu.

Ripoti zinaonyesha kuwa magenge haya mara nyingi huajiri vijana waliokata tamaa kimaisha, wanaokosa ajira, au walioathirika na dawa za kulevya.

Hii ndio hali inayoshuhudiwa pia katika baadhi ya maeneo ya Pwani kama Kisauni na Likoni, ambako magenge ya vijana wadogo yameibuka na kuanzisha mitandao ya wahalifu.