Hofu utabiri ukionyesha mvua itapungua maeneo ya kati ya Kenya
SERIKALI za kaunti zilizo katikati mwa Kenya, zimekumbwa na hofu baada ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Nchini kutabiri kuwa zitapata mvua ya chini ya wastani msimu ujao.
Kulingana na idara hiyo ya hali ya hewa, kaunti za eneo hilo, zikiwemo Nyandarua, Murang’a, Nyeri na Laikipia, huenda zikawa na mvua ya chini kuliko kawaida msimu wa mvua ya masika ambao kwa kawaida huanza Machi hadi Mei.
Utabiri huo umesababisha wasiwasi kutokana na athari zake kwa kilimo na upatikanaji wa maji.Kaunti kama vile Nyandarua na Nyeri tayari zinatoa onyo kutokana na uhaba wa vyakula muhimu.
Hii inachangiwa na kiwango kidogo cha mvua ya vuli mwishoni mwa mwaka jana (Oktoba hadi Novemba), ambayo ilisababisha mavuno kupungua.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Kaunti za Nyeri, Murang’a na Nyandarua zinaepuka mahindi na maharagwe kwa mazao ya kibiashara zaidi na kukuza mimea inayostahimili ukame na inayochukua muda mfupi kukomaa kama vile mboga na alizeti.
Katika Kaunti ya Murang’a, serikali ya Gavana Irungu Kang’ata kwa ushirikiano na kampuni ya Kenya Breweries Limited inakuza kilimo cha mtama kama mumea wa kibiashara.
Waziri wa Kilimo, Biashara na Viwanda katika kaunti hiyo, Kimani Mugo, anasema mtama unakuzwa katika sehemu kavu za kaunti ikiwa ni pamoja na Kambiti, Maragua, Kakuzi, Kiharu na sehemu za chini za Gatanga.
“Mtama ni zao linalostahimili ukame, na kama kaunti, tunahakikisha kwamba wakulima wanapata mbegu zilizoidhinishwa. Chini ya maagizo ya mkuu wa kaunti, idara imeteua kikosi maalumu cha maafisa wa kilimo kuongoza na kuhakikisha kuwa wakulima wanazingatia kanuni bora za kilimo.
Anasema kuwa mtama ni miongoni mwa mazao yaliyosahaulika licha ya kuwa na thamani kubwa ya lishe na biashara.Idara ya Kilimo katika Kaunti ya Nyeri inajitahidi kuepuka tatizo la chakula.
Wakati wa msimu wa mvua mwishoni mwa mwaka jana, kaunti ilipokea wastani wa milimita 251 kwa siku 26 kuanzia wiki ya mwisho ya Oktoba.
“Mvua, ambayo ilikuwa chini ya kiwango cha asilimia 41, haikuwa ya kutosha kwa uzalishaji wa mazao, na kusababisha kupungua kwa mavuno,” anasema Waziri wa Kaunti anayesimamia Fedha, Robert Thuo, ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Kilimo.
Anaeleza kuwa mvua hiyo ilisababisha kupungua kwa ekari zinazokuzwa mahindi kwa hektari 328.Kwa sasa, akiba ya mahindi huko Nyeri ni magunia 7,636 dhidi ya mahitaji ya matumizi ya magunia 16,715 kwa mwezi.