Hospitali za rufaa sasa kujengwa Kericho, Bungoma
UKANDA wa Kusini mwa Bonde la Ufa unatarajiwa kuwa na hospitali ya pili ya mafunzo na rufaa baada ya Baraza la Mawaziri kuidhinisha ujenzi wa vituo vya afya vya Level VI kwenye kaunti za Kericho na Bungoma.
Kwa sasa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru ndiyo hospitali kubwa zaidi kwenye ukanda wa Kusini mwa Bonde la Ufa.
Hospitali hii huhudumia wagonjwa kutoka Nakuru na kaunti sita za Kericho, Nyandarua, Baringo, Narok, Laikipia na Samburu.
Wale ambao huathirika na visa vya ujangili kwenye kaunti za Samburu, Baringo na Laikipia huwa wanasafirishwa hadi Nakuru ili kupokea matibabu spesheli.
Hospitali ya Nakuru ina kituo kikuu cha kutibu maradhi ya Kansa na kitengo cha sasa cha kujifungua watoto ambacho kina vitanda 250 na kinafahamika kama Margaret Kenyatta.
Viongozi wa Kaunti ya Kericho wamependekeza hospitali hiyo mpya ijengwe mjini Londiani.
Uamuzi wa kujenga hospitali hiyo unalenga kuimarisha miundomsingi kwenye kaunti ambazo wakazi wake wamekuwa wakipambana kupata huduma bora za kimatibabu.
Kwa mujibu wa Baraza la Mawaziri, hospitali zitakazojengwa Kericho na Bungoma zitapanua huduma za afya na kuhakikisha wanaohitaji huduma spesheli za matibabu wanazipata karibu na raia.
Kenya ina zaidi ya hospitali nane za mafunzo na rufaa ambazo ni Kenyatta (KNH), Moi (MTRH), Jaramogi (JOOTRH), Nakuru (NTRH), Kisii (KTRH), Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRH), Mathari (MNRTH) na Hospitali inayotibu majeraha ya mgongo, (NSIH).