IEBC: Vijana walia kufungiwa nje mahojiano ya kumteua mwenyekiti, makamishna wa IEBC yakianza Jumatatu
HUKU mahojiano ya kumteua mwenyekiti na makamishna wapya sita wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) ya
kitarajiwa kuanza rasmi Machi 31, 2025, vijana sasa wanalia kufungiwa nje.
Mwenyekiti wa shirika la Kenya Youth Johnmark Ababu, anadai kuwa vijana wengi walituma ombi lao ila hakuna hata moja aliyebahatika.
“Baadhi ya watu ambao majina yao yaliorodhoshwa ni wazee. Hakuna hata kijana mmoja katika orodha hiyo,” alisema Bw Ababu.
Kando na hayo, shirika hilo linampinga sana Charles Nyachae ambaye analenga wadhifa wa uenyekiti wa tume ya IEBC.
Bw Nyachae ni mmoja wa watu ambao watafanyiwa mahojiano siku ya Jumatatu ili kupata mrithi wa aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati aliyeaga dunia mwezi jana.
Shirika hilo linadai kuwa Bw Nyachae hafai kushikilia wadhifa huo kutokana na masuala mbalimbali.
“Pingamizi hilo liliwasilishwa katika risala ya Machi, 17, 2025, iliyoelekezwa kwa mwenyekiti wa jopo la uteuzi wa IEBC. Pingamizi hilo linazua wasiwasi mkubwa kuhusu kufaa kwa Nyache kwa jukumu hili muhimu, na kusisitiza umuhimu wa uadilifu na viwango vya maadili katika mchakato wa uchaguzi nchini Kenya,” akasema Bw Ababu.
Naye Mourice Masiga, katibu wa shirika hilo anasema kuwa vijana wanafaa kupewa nafasi kama hizo kwani wana uwezo na tajriba hitajika.
“Rais amekuwa akituahidi kuwa vijana watajumuishwa na hata kuteuliwa katika vitengo mbalimbali ila hilo halijafanyika bado,” akasema Bw Masiga.
Shirika hilo pia limetishia kuandaa maandamano Jumatatu ikiwa mchakato huo utaendelea bila matakwa yao kushughulikiwa.
Aliyekuwa msajili wa Idara ya Mahakama Anne Amadi, Charles Nyachae na Mwenyekiti wa Bodi ya Kawi Joy Brenda Mdivo ni miongoni mwa wagombeaji 11 walioteuliwa kuwania nafasi ya uenyekiti wa IEBC.
Kufikia Machi 6, 2025, jumla ya watu 1,356, wakiwemo wanasiasa, maafisa wa zamani wa serikali na watu wenye uhusiano na Rais William Ruto na Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, walikuwa wametuma maombi ya kuteuliwa katika nyadhifa hizo.
Kati ya hao, 37 walitaka uenyekiti, huku 1,319 wakitaka kuwa makamishna.