IPOA yaelezea changamoto katika kukabili dhuluma za kijinsia miongoni mwa polisi
MAMLAKA Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA) imeelezea changamoto kubwa katika kukabiliana na masuala ya dhuluma za kingono na pia kijinsia miongoni mwa maafisa wa polisi.
Katika mahojiano na wanahabari baada ya kuzindua warsha iliyoandaliwa na shirika la FEMNET kuangazia masuala ya haki za kijinsia na afya ya uzazi jijini Nairobi, Machi 4, 2025, Naibu Mwenyekiti wa IPOA, Bi Anne Wanjiku Mwangi, alisema changamoto kuu ni kukosa ushirikiano hasa kutoka kwa maafisa wakuu.
“Tunapokuwa na afisa wa polisi ambaye amefanya kitendo hicho hasa kwa wanaozuiliwa, au kuwadhulumu wake wao, tuna tatizo la kukosa ushirikiano, ambapo yule anayesimamia hawezi kutoa taarifa zinazohitajika na stakabadhi kutuwezesha kuendelea na kesi,” akasema.
“Changamoto nyingine ni kwamba huwa tuna kesi ambazo zinafika kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (ODPP) na kesi hizo zinahitaji kufikishwa kortini. Lakini kwa sababu ya mrundiko wa kesi katika ODPP, inachelewesha kesi hizi kushughulikiwa,” anaeleza.
Hata hivyo, Bi Mwangi anasisitiza kuwa wanafuatilia masuala hayo kuhakikisha haki inatendeka.
“Tumejitolea kufuatilia haya kwa sababu ni ukosefu wa haki hasa tunapokuwa na mwanamke katika kituo cha polisi labda akitafuta haki na kisha kuishia kudhulumiwa hapo,” anasema.
Visa vya dhuluma za kingono miongoni mwa polisi, vilikuwa juu zaidi eneo la Magharibi, katika ziara ambayo IPOA ilifanya majuzi katika maeneo ya humu nchini, anasema.
“Katika eneo hili, tulikuwa na visa saba ambavyo kwangu mimi ni vingi huku maeneo mengine yakiwa na kisa kimoja au viwili. Lakini Magharibi mwa Kenya ni jambo ambalo tunafuatilia kwani ni dhuluma za kingono zilizotekelezwa na polisi,” anaongeza.
“Kwa hivyo, tunashughulikia kuunda sehemu salama ambapo tunahamasisha maafisa wa kiume na pia kike, kuhusu Sheria dhidi ya Dhuluma za Kingono. Hii ni kwa sababu wao ndio wanahitajika kuwalinda watoto wetu,” anasema.
Naibu mwenyekiti huyo wa IPOA alifichua hayo huku Mkurugenzi Mkuu wa FEMNET Bi Memory Kachambwa akihimiza mdahalo kuhusu masuala ya haki za kijinsia na afya ya uzazi baadhi ambayo yamepuuzwa au kukosa kupewa uzito.
Wawakilishi kutoka mataifa zaidi ya 15 barani Afrika wamekutana kwa warsha hiyo, kujadili masuala kwa lengo la kuunda mfumo ambao utatoa mwelekeo kuhusiana na masuala ya kijinsia, afya ya uzazi na haki husika.
FEMNET inaeleza kuwa hata ingawaje kuna juhudi kadha zilizopigwa kushughulikia masuala hayo, bado kuna changamoto zinazohitaji suluhu kwa kuwa baadhi zinakabiliwa na pingamizi tofauti kutokana na misimamo ya kidini, kitamaduni, sera kandamizi miongoni mwa masuala mengine.
Kulinganana Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), haki hizi za masuala ya kijinsia na afya ya uzazi ni pamoja na ufikiaji wa mbinu za upangaji uzazi, matibabu ya uzazi, afya ya wajawazito, kupata tiba ya maradhi ya zinaa, kulindwa dhidi ya dhuluma za kijinsia na elimu ya mahusiano salama.
Pia inaeleza kuwa upataji wa huduma za afya ya uzazi ni haki za kibinadamu ambazo, lengo lake sio kuwa na afya iliyoimarika pekee, bali pia inachangia katika usawa wa kijinsia na maendeleo kwa jumla.