Habari za Kitaifa

Itisha Sh3, 000 za kupigia Ruto makofi ziarani Mlima Kenya – Gachagua ashauri wakazi

Na CHARLES WASONGA March 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rais Rigathi Gachagua amewashauri wakazi wa Mlima Kenya wasikubali kuhongwa pesa kidogo ili wamlaki Rais William Ruto, akiwataka waitishe “pesa nzuri”.

Akiongea Jumamosi, Machi 29, 2025 mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru alipohudhuria sherehe ya kutawazwa kwa Kasisi Harrison Munyua wa Kanisa la Redeemed Gospel, Bw Gachagua alidai pesa zimepelekwa kwa magunia kuhonga wakazi wasimwaibishe Rais kwa kumzomea bali wamkaribishe kwa furaha.

Aliwasihi wachukue pesa hizo lakini wasiamini yale ambayo Rais Ruto atasema kwa sababu, kulingana naye, sio ya kweli.

“Msikubali Sh200 ili mjitokeze kusikiza uongo. Tukubaliane kwamba mtaitisha Sh3, 000 na akina mama watakaopiga shangwe wanapaswa kulipwa Sh10, 000 na wanaopiga makofi wanapasa kulipwa Sh2, 000,” Bw Gachagua akashauri.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa zamani wa Mathira aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kutojumuisha pesa hizo na zile ambazo walichuma kwa jasho, bali wazitumie kulipia madeni yao na kwa matumizi mengine ya kawaida.

“Msipeleke hizo pesa nyumbani, mzitumie sokoni kwa sababu ni pesa za laana. Aidha, mtumie kulipa madeni ya “shylocks” na wakopeshaji kwa njia ya simu. Msichanganye pesa hizo na zile zenu za zamani wala kutumia kulipia karo au kununua mifugo,” akaongeza.

Bw Gachague alieleza kuwa ni sawa kwa wakazi wa Mlima Kenya kupewa pesa “kwa sababu watu wetu walimuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa 2022 bila kuitisha chochote.”

Wiki iliyopita Rais Ruto alikutana, katika Ikulu ya Nairobi, na wanasiasia, mawaziri, makatibu wa wizara na maafisa wengine wa serikali kutoka Mlima Kenya kupanga mikakati ya ziara yake ya siku sita inayoanza Jumanne, Aprili 1, 2025.

Aidha, Naibu Rais Kithure Kindiki, wabunge na maafisa wengine wa Serikali walizuru maeneo ya mashinani kufanya maandalizi ya ziara hiyo na kurai wakazi kumpa Rais Ruto mapokezi mazuri.

Isitoshe, mabango makubwa yenye jumbe za kumkaribisha Rais Ruto yametundikwa katika miji mbalimbali ya Mlima Kenya ikiwemo Kiambu, Nyeri, Kerugoya, Embu na kandokando mwa barabara kuu ya Thika – Thika Road.

Ziara ya kiongozi wa taifa itaanza katika kaunti ya Laikipia, kisha aelekee Meru, Kirinyaga, Nyandarua, Murang’a, Tharaka Nithi na Embu.

Katika siku ya mwisho ya ziara hiyo, Aprili 5, 2025 Rais Ruto atazuru kaunti za Nyeri na Kiambu.

Rais Ruto hajafanya ziara ya kukutana na watu na kukagua miradi ya maendeleo Mlima Kenya tangu Oktoba mwaka jana Bw Gachagua alipotimuliwa afisini.

Kutimuliwa kwa kiongozi huyo kuliwakasirisha wakazi kwani walichukulia kitendo hicho kama usaliti.

Aidha, wakazi wa Mlima Kenya hawajafurahia handisheki ya Rais Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wakidai ni njama ya kutenga eneo lao kimaendelea na kuwafuta kazi watu kutoka Mlima Kenya wanaoshikilia nyadhifa kubwa serikalini.

Mara ya mwisho Dkt Ruto kufika eneo la Mlima Kenya ilikuwa Novemba 16, 2024 alipohudhuria sherehe ya kutawazwa kwa Askofu Peter Kimani Ndung’u kuwa Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Embu.

Rais alizomewa na wananchi katika hafla hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Embu na kuhudhuriwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Bw Gachagua na Profesa Kindiki.

Mnamo Desemba 8, 2024, Dkt Ruto pia alimtembelea Bw Kenyatta nyumbani kwake katika kijiji cha Ichaweri, Gatundu Kusini, Kiambu.

Hata hivyo, alisafiri kwa helikopta ili kukweka kukutana ana kwa ana na wanachi.

Tangu wakati huo, wandani wake Rais wamekuwa na wakati mgumu kumtetea na hata kuwasilisha jumbe na michango yake katika hafla za makanisa na mazishi.

Kwa mfano, Januari mwaka huu wananchi walimzuia aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi kusomewa risala za rambirambi kutoka kwa Dkt Ruto katika mazishi ya mwana wa aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Kivuti.