Jaji aondoa jina la Rais Ruto katika kesi ya utekaji nyara
JAJI mmoja wa Mahakama Kuu, ameondoa jina la Rais William Ruto kutoka kesi inayohusiana na uharibifu wa mali wakati wa maandamano, na utekaji nyara wa raia.
Kesi hiyo, ambayo Mwanasheria Mkuu aliitaja kama isiyoeleweka, iliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Eldoret Juni 2024.
Hii ilikuwa katika kilele cha maandamano ya vijana kupinga serikali, kudai utawala bora na kukomeshwa kwa ufisadi serikalini.
Bi Rodah Cheptarus, mlalamishi katika kesi hiyo, aliomba mahakama kutoa maagizo kadhaa, ikiwemo kwamba “Jina la Rais, pamoja na bendera na nembo ya Jamhuri ya Kenya, linapaswa kulindwa na halifai kutumiwa kwa maslahi ya kibinafsi.”
Bi Cheptarus alimshtaki Rais na Mwanasheria Mkuu, Rais akiwa mshtakiwa wa kwanza na Mwanasheria Mkuu mshtakiwa wa pili.
Hata hivyo, Jaji Reuben Nyakundi aliamua kwamba kesi hiyo ilikuwa na lengo la kuondoa kinga ya Rais dhidi ya mashtaka ya kisheria.
Alifuta jina la Rais kwenye kesi hiyo baada ya Mwanasheria Mkuu kupinga, akisema kuwa Rais hawezi kushtakiwa binafsi kwa kuwa ana kinga dhidi ya mashtaka yoyote ya kisheria.
“Ni uamuzi wangu kwamba isipokuwa kwa hali zilizoruhusiwa chini ya sheria, Rais aliye madarakani hawezi kuwa mshiriki katika kesi yoyote ya kisheria mahakamani. Hoja yoyote inayopendekeza uwezekano wa kumhusisha Rais kama mshiriki wa kesi ili maagizo ya mahakama yatolewe, kwa kweli, haizingatii masharti ya Ibara ya 143 ya Katiba,” alisema Jaji Nyakundi katika uamuzi wake wa tarehe Aprili 2, 2025.
Alifafanua: “Chini ya mfumo wetu wa kutenganisha madaraka, aina ya mamlaka ya urais inampa Rais kinga kamili dhidi ya mashtaka ya jinai au madai yanayohusiana na mamlaka yake ya kikatiba.”
Jaji alisisitiza kuwa kinga inayotolewa katika Ibara ya 143 ya Katiba inaisha mara tu Rais anapomaliza muda wake ofisini.
Aliamuru kesi hiyo iendelee dhidi ya Mwanasheria Mkuu kama mshtakiwa mkuu.