Habari za Kitaifa

Jinsi Ruto alichezea shere wasichana na wanawake, ahadi ya sodo bado ndoto

Na KAMAU MAICHUHIE June 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAJIRA ya asubuhi mnamo Juni 10, 2022, William Ruto, ambaye alikuwa Naibu wa Rais wa Kenya, alitia saini mkataba wa kulinda maslahi ya wanawake ulioorodhesha sera za kuwainua akina mama nchini endapo angeshinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Shughuli hiyo ilifanyika katika uwanja wa Michezo wa Nyayo, Nairobi.

Ilikuwa na msisimko mkubwa ikihudhuriwa na maelfu ya wanawake wafuasi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) waliovalia mavazi na vitambaa vyenye rangi ya chama hicho.

Dkt Ruto alishinda katika uchaguzi huo na kuwatazwa rais wa tano wa Kenya, ikiaminika kuwa sehemu ya kura alizopata zilichangiwa na wanawake na wasichana waliovutiwa na ahadi nyingi alizowapa.

Mkataba wa Kenya Kwanza kuhusu Wanawake uliahidi kuimarisha ujumuishaji wa wanawake katika nyanja za siasa na uchumi.

Kwanza, ilikuwa ni utekelezaji wa kanuni ya usawa wa kijinsia unaohakikisha kuwa angalau thuluthi moja ya nafasi kuu za kuchaguliwa na kuteuliwa serikalini zinashikiliwa na wanawake.

Dkt Ruto aliahidi kutimiza ahadi hiyo siku 100 baada ya kuingia afisini.

Ndoto ya kutekelezwa kwa kanuni hiyo ya usawa wa jinsia iliyashinda mabunge ya awamu ya 10, 11, na 12, huku miswada iliyolenga kufikia hilo ikifeli kupitishwa na idadi tosha ya wabunge.

Ili kufikia ahadi hii, Dkt Ruto alilenga kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na asasi zingine kuhakikisha kuwa teuzi zote za umma zinatimiza hitaji hilo la usawa wa kijinsia.

Dkt Ruto pia aliahidi kutenga asilimia 50 ya nafasi za uwaziri kwa wanawake.

Aidha, aliahidi kuanzisha mpango wa kutoa sodo na fyambo (diapers) kwa wanawake waliojifungua ndani ya miezi mitatu ya kwanza baada ya kuzaa.

“Kutakuwa na mwamko mpya katika uongozi wa taifa la Kenya, ambapo wanawake wataweza kuketi katika meza sawa na wanaume.
“Wanawake watakuwa washirika sawa. Wanawake watapata sauti, usemi na nafasi sawa katika asasi kuu ya kufanya maamuzi makuu serikalini. Tutaondoa huu mtindo wa wanawake kupewa zawadi ndogo na za kudunisha na kuhakikisha kuwa wanawake wanashikilia nafasi sawa katika uongozi wa taifa hili,” Dkt Ruto akasema siku hiyo mbele ya maelfu ya wanawake waliojawa na matumaini makuu.

Aliahidi kuwa kufikia Desemba 2002, kila mwanamke nchini angepewa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) kwa gharama nafuu.

Kuhusu elimu, Kenya Kwanza iliahidi kuendeleza sera ya kuhakikisha kuwa wasichana wote waliopata uja uzito kabla ya kukamilisha masomo wanapewa nafasi ya kuendelea na masomo chini ya mpango wa basari unaofadhiliwa na serikali.

Wajane na akina mama wasio na waume hawakuachwa nyuma kwani Kenya Kwanza iliahidi kutekeleza sera za kujali maslahi yao.

“Tutaanzisha sera ya kulinda wanawake wenye umri mkubwa, wajane, akina mama wasio na waume, wasichana mayatima na wanawake walemavu,” Dkt Ruto akaeleza.

Aidha, aliahidi kuwa serikali yake ingeanzisha hazina maalum ya kuwasaidia wajane wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumu, na kuhakikisha kuwa wanawake wasio na waume wanapata basari ya watoto wao kutoka kwa serikali bila vikwazo vyovyote.

Lakini siku 1,000 baada ya kuingia mamlakani Rais Ruto hajapiga hatua katika kutekeleza ahadi alizotoa kwa wanawake wakati wa kampeni za 2022.

Uchunguzi wa Taifa Leo unaonyesha kuwa ahadi nyingi za Rais kwa wanawake na wasichana hazijatimizwa.

Kwanza, utekelezaji wa kanuni ya kuhakikisha kuwa angalau thuluthi moja ya nyadhifa za umma zinashikiliwa na wanawake ndani ya siku 100 haujatimizwa.

Mnamo Juni 2023, taifa lilipata matumaini kuwa kanuni ya usawa wa kijinsia ungetimizwa baada ya aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Aisha Jumwa kuteua Jopo kazi la Kushughuli Kanuni ya Usawa wa Kijinsia.

Hata hivyo, hata baada ya jopo kazi hilo mnamo Aprili mwaka jana, kuwasilisha ripoti yenye mapendekezo kuhusu njia za kufikiwa kwa usawa wa kijinsia Bungeni, hakuna hatua imechukuliwa kufikia hilo.

Bi Daisy Amdany, mkurugenzi mkuu wa Shirika la CRAWN Trust, anasema inasikitisha kuwa kanuni kuhusu usawa wa kijinsia haujatimizwa hadi sasa.

“Rais hajachukua hatua yoyote licha ya kwamba bunge limepokea ripoti yenye mapendekezo yetu kuhusu njia ya kutekeleza kanuni hii. Lakini Rais Ruto amekuwa akiahidi kwamba kufikia mwisho wa muhula wake wa kwanza uongozini atatimiza ahadi hiyo. Lakini hamna mswada wa sheria uliwasilishwa bungeni kufanikisha hilo,” Bi Amdany anaambia Taifa Leo.

Ahadi ya kugawa nyadhifa za uwaziri kwa usawa (asilimia 50-50) baina ya wanaume na wanawake pia haijatekelezwa na Rais Ruto.
Alipoteua mawaziri wake mnamo Septemba 2022, Ruto alitenga chini ya asilimia 30 pekee ya nafasi za uwaziri kwa wanawake.

Baraza lake la kwanza la mawaziri lilikuwa na wanawake saba pekee, likisalia na nafasi nne litimize kanuni ya kikatiba kwamba angalau thuluthi moja ya mawaziri wawe wanawake.

Rais Ruto amefeli kutimiza ahadi hiyo (ya kuhakikisha kuwa asilimia 50 ya nafasi za uwaziri zinashikiliwa na wanawake) hata baada ya kutekeleza mabadiliko katika baraza lake la mawaziri mara kadhaa tangu kufanyika kwa maandamano ya Gen Z ya Juni, 2024.

Idadi ya wanawake katika baraza la mawaziri ingali chini kiasi kwamba wanashikilia nafasi nane pekee miongoni mwa mawaziri 26, idadi inayowakilisha asilimia 28 pekee.

“Kuhusu ahadi kwamba nusu ya idadi ya mawaziri wangekuwa wanawake, Rais Ruto hajaitimiza. Aidha, amefeli kutimiza hilo katika uteuzi wa makatibu wa wizara, mabalozi na teuzi zingine kuu serikali,” Bi Amdany anaongeza.

Isitoshe, karibu miaka mitatu baada ya Rais Ruto kuingia Ikulu wanawake waliojifungua na wasichana bado wanasubiri ‘diapers’ na sodo bila malipo, mtawalia.

Kuhusu mpango wa utoaji ‘diapers’ bila malipo kwa wanawake waliojifungua kwa kipindi cha miezi mitatu ya kwanza, hamna kinachofanywa na serikali kutimiza ahadi hiyo, anaongeza Dkt Amdany.

“Kwa hivyo, ninasema kuwa ahadi hiyo haijatimizwa,” akasisitiza.

Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, mkosoaji mkuu wa utawala wa Kenya Kwanza anaambia Taifa Leo kwamba kwani inasikitisha kuwa ahadi nyingi ambayo Dkt Ruto alitoa kwa wasichana na wanawake wa taifa hili hazijatimizwa.