Habari za Kitaifa

Joho aepuka kusukumwa jela miezi sita majaji wakifuta adhabu

Na ANTHONY KITIMO November 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa madini na uchumi wa majini, Hassan Joho, amepata afueni baada Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali hukumu ya mahakama ya Mazingira na ardhi iliyomtaka kufungwa jela kwa miezi sita kwa kukaidi amri ya mahakama.

Uamuzi huo wa korti ya rufaa ni pigo kubwa kwa bwenyenye Ashok Doshi na mkewe Pratibha Ashok ambao walitaka Bw Joho na mwakilishi wadi wa Changamwe George Ogutu kufungwa jela kwa kutotii mahakama.

Katika hukumu iliyotolewa na Majaji Agnes Murgor, Jessie Lesit na George Odunga, walitupilia mbali hukumu iliyotolewa na Jaji Sila Munyao wa mahakama ya mazingira na ardhi April 22 2020.

“Mahakama imepata kuwa walalamishi (Bw Doshi na mkeo Pratibha) hawakuonyesha ushahidi kuwa waliwasilisha amri ya mahakama kwa Bw Joho na Bw Ogutu kufika mahakamani, hivyo basi, korti imetupilia mbali hukumu iliyotolewa Februari 12 2020,” majaji walisema katika uamuzi waliotoa Novemba 8 2024.

Mahakama hiyo pia iliamrisha Bw Doshi na mkewe kugharamia gharama ya rufaa hiyo. Doshi na mkewe Pratibha, walikuwa wamelalamika kuwa Bw Joho na Bw Ogutu walikiuka agizo la mahakama lililozuia serikali ya Kaunti ya Mombasa kuingia bila ruhusa katika shamba lao.

Kupitia wakili Willis Oluga, mfanyibiashara huyo na mkewe walisema kuwa mnamo Mei 10 2019, maafisa wa serikali ya kaunti wakiongozwa na Bw Joho na viongozi wengine wa Mombasa walivamia ardhi hiyo na kuvunja lango. Waliongeza kuwa viongozi hao pia walifanya mkutano wa umma ambapo walimshtumu Bw Doshi kuwa mnyakuzi wa ardhi.

Kupitia wakili Murtaza Tajbhai, Bw Joho aliiambia mahakama kuwa hakuwa amepewa agizo hilo la mahakama. Bw Doshi na mkewe pia wanataka agizo la kudumu la kuzuia serikali ya kaunti na Bw Ogutu au mtu yeyote kuvunja ukuta au nyumba yoyote katika ardhi hiyo.

Wanaongeza kuwa madai ya kuwa ardhi hiyo ilikuwa imenyakuliwa kutoka kwa shule hayana msingi wowote sababu hatimiliki na umiliki ya awali ilikuwa imethibitishwa na mahakama mbalimbali.

Mfanyibiashara huyo na mkewe wanateta kuwa kando na kuvamia ardhi hiyo na kusababisha uharibifu mkubwa, serikali ya kaunti ilitishia kuwafurusha kwa nia ya kurejesha umiliki wa ardhi hiyo kwa shule ya upili ya Changamwe.