Joho ashangaza wabunge kwa kujieleza kwa ufasaha lugha ya Kiingereza
WAZIRI Mteule wa Uchumi wa Maji, Uchimbaji wa Madini na Rasilimali za Majini Hassan Ali Joho Jumapili aliwashangaza wabunge alipojieleza kwa ufasaha kwa lugha ya Kiingereza na kudhihirisha ufahamu mpana kuhusu masuala ya wizara hiyo licha madai kuwa hajahitimu kimasomo.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah aliibua kicheko, katika kikao cha kumhoji Bw Joho, aliposema kuwa “hata Wakenya wengi wameshangaa kuwa Joho anaweza kuzungumza lugha ya Kiingereza.”
Gavana huyo wa zamani wa Mombasa alikiri kuwa alipata gredi ya D- katika mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mnamo 1993 lakini hiyo haijamzuia kupata shahada ya uzamili.
Akipuuzilia madai kuwa hana shahada halali ya digrii akieleza mnamo 2013 alihitimu kwa shahaha ya digrii katika Chuo Kikuu cha Kampala baada ya kusomea shahada ya diploma “kuboresha gredi yangu ya D-.”
“Baada ya hapo nilisomea shahada nyingine ya digrii katika taaluma ya Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kuu cha Gretsa iliyoko Thika kaunti ya Kiambu. Baada ya hapo nilisomea Shahada ya Digrii ya Uzamili katika taaluma ya Uongozi katika Chuo Kikuu cha ‘Harvard Kennedy School of Government” na nikafuzu”, Bw Joho akaambia Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi akipigwa msasa kubaini ufaafu wake kuhudumu kama Waziri Serikalini.
“Ndio nilipata gredi ya D- katika mtihani wa KCSE. Lakini sikuvunjika moyo, niliweza kuendelea kukwea ngazi ya masomo na sasa niko na shahadi za uzamili kutoka chuo kikuu chenye hadhi ya juu zaidi duniani,” Bw Joho akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.
Aliwaeleza wabunge kwamba hali hiyo ilichangiwa na umasikini uliozonga familia yake, kiasi kwamba nyakati fulani alilazimika kukatiza masomo yake kwa mwaka mmoja kufanya biashara ili apate karo.
Alikuwa akijibu maswali kutoka kwa kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah na kiranja wa wachache Junet Mohamed kuhusu suala la uhalali wa elimu yake.
Bw Joho alieleza kuwa wale wanaotilisha shaka uhalali wa masomo yake ni maadui wake wa kisiasa “wakiongozwa na Mzee mmoja wa Mombasa mwenye umri wa miaka 82.”
“Lakini Mheshimiwa Spika nataka kuihakikishia kamati hii kwamba endapo nitarejea hapa tena kupigwa msasa nitakuwa nimepata shahada ya uzamifu (PhD) na nitakuwa nikitambuliwa kama Dkt Joho,” akaeleza.
Gavana huyo wa zamani wa Mombasa alisema kuwa alitiwa shime na moyo masomoni na msomi mashuhuri Profesa Ali Mazrui ambaye hakufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne “lakini hiyo haikumzuia kuendelea kimasomo hadi kuwa Profesa wa taadhima kubwa”.
Aidha, Bw Joho aliwaacha wabunge vinywa wazi alipoelezea kwa undani maono yake kwa Wizara hiyo na jinsi atakavyopambana na magenge ya matapeli katika sekta ya madini.
“Kuna wanaojifanya kufanya uchunguzi kuhusu uwepo wa madini kwa miaka 40. Hii haiwezekani. Tunahitaji kuangaliwa upya sera zinazoongoza sekta hii ya madini. Nitaanzisha sera bora zitakazoiwezesha kuchangia zaidi ya asilimia 1 ya mapato ya kitaifa ilivyo sasa,” Bw Joho akaeleza kwa ufasaha hali iliyomfurahi Mbunge wa Tharaka George Gitonga Murugara.
Gavana huyo wa zamani wa Mombasa pia aliweka wazi mikakati atakayotekeleza kufufua sekta ya uvuvi katika Bahari Hindi, Ziwa Victoria na maziwa mengine nchini.
“Ndani ya miaka mwaka mmoja nitahakikisha kuwa Kenya inauza zaidi ya tano 10 zaidi ya samaki katika masoko ya ng’ambo,” Bw Joho akasema.
Gavana huyo wa zamani wa Mombasa alikana madai kuwa anahusika katika ulanguzi wa mihadarati.
Bw Joho alisema kuwa hakuna ushahidi kwamba wowote ambao umewasilishwa na asasi yoyote ya umma kumhusisha na uovu huo.
Alieleza kuwa wakati mmoja, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani marehemu Profesa George Saitoti aliwasilisha ripoti bungeni ambayo ilimwondolea lawama kuhusu madai kuwa alihusika katika sakata ya ulanguzi wa dawa za kulevya.
“Ni kweli kwamba madai hayo yamewahi kutolewa dhidi yangu. Uchunguzi ulifanywa na asasi husika za serikali. Baadaye aliyekuwa waziri wa usalama Profesa Saitoti aliwasilisha bungeni ripoti hiyo ya uchunguzi ulioendeshwa na asasi za humu nchini na kimataifa na hakukuwa na ushahidi wowote wa kunihusisha na madai hayo,” Bw Joho ambaye alifichua kuwa thamani ya utajiri wake ni Sh2.36 bilioni.
Mawaziri wengine waliopigwa msasa jana ni; Alfred Mutua (Leba), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Justin Muturi (Utumishi wa Umma).