Kagwe, Kabogo na Kinyanjui wateuliwa mawaziri serikalini
RAIS William Ruto ameteua Mutahi Kagwe kama Waziri wa Kilimo, Lee Kinyanjui kama Waziri wa Biashara na William Kabogo kama Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano katika mabadiliko ya hivi punde.
Katika uteuzi huo ambao umejiri juma moja na nusu tangu handisheki baina ya Rais Ruto na [Rais Mstaafu] Uhuru Kenyatta, umesheheni pia mageuzi mengine yaliyomtoa Kipchumba Murkomen kutoka kwa Wizara ya Michezo hadi kwa Wizara ya Usalama wa Ndani iliyokuwa inashikiliwa na Kithure Kindiki kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Rais.
Wakati huo huo, aliyekuwa waziri wa michezo Ababu Namwamba ameondolewa kwenye kibaridi kikali cha kuwa nje ya serikali, kwa kuteuliwa kuwa balozi wa Kenya katika shirika la Unep. Naye mwanauchumi Ndiritu Muriithi, ambaye ni mwandani mwingine wa Uhuru, ameteuliwa mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru, KRA.
Kembi Gitura, ambaye pia ana ukaribu na rais mstaafu amepewa kiti cha Olive Mugenda, aliyekuwa mwenyekiti wa hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Wengine walioathiriwa na mabadiliko ni Andrew Karanja, ambaye aliteuliwa Waziri wa Kilimo majuzi tu, ambaye sasa atakuwa Balozi wa Kenya nchini Brazil.
Waziri Salim Mvura naye amehamishwa hadi Wizara ya Michezo huku Dorothy Angote akiteuliwa Balozi wa Kenya nchini Zimbabwe.
Gumzo kuhusu wandani wa Uhuru kuingia serikalini lilishika wiki jana baada Rais Ruto kumtembelea Bw Kenyatta nyumbani kwa Ichaweri, Gatundu Kusini ambapo walipigwa picha wakiwa katika handisheki.
Habari zilisema baadaye kwamba Ruto alipeleka mbuzi 12 kama zawadi na maridhiano, kulingana na mila za Agikuyu.