Kalonzo akataa chanjo ya mifugo
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amewataka Wakenya kukataa mpango wa kitaifa wa utoaji chanjo kwa mifugo nchini.
Alisema zoezi hilo limefadhiliwa na taasisi za kigeni za utafiti zinazolenga kuanzisha dawa za kubadilisha msimbojeni (DNA) kwa mifugo nchini.
Wiki jana, Rais William Ruto alisema jumla ya ng’ombe milioni 22 na mbuzi na kondoo milioni 50 watapewa chanjo ya lazima kwa lengo la kuimarisha afya yao.
Kiongozi wa nchi alisema hatua hiyo itawezesha baadhi za mifug kutoka Kenya kununuliwa kwa urahisi katika masoko ya kimataifa.
Lakini Ijumaa, Novemba 15, 2024 Bw Musyoka alisema kampeni hiyo ya utoaji chanjo imekataliwa katika nchi mbalimbali ulimwenguni.
“Chanjo hii itabadilisha msimbojeni kwa mifugo na madhara yake yanaweza kujitokeza baada ya miaka mingi kupitia kuzalishwa wanyama wenye viungo vilivyo na hitilafu,” akasema.
“Watu wanaoleta chanjo hiyo nchini huwaendeshi mipango hiyo katika nchi zao, ambako kuna mifugo wengi kuliko Kenya na hivyo ndio wanachama wakubwa wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Tunajua kuwa chanjo hizo zimekataliwa hata kwao kule Amerika,” Bw Musyoka akasema.
Kinara huyo wa Wiper aliyewahutubia wanahabari jijini Nairobi, akiandamana na viongozi wenzake wa upinzani, alisema serikali inaendesha chanjo hiyo kwa lengo la kutumia sekta ya mifugo nchini.
“Baada ya kufanya hivyo, wao ndio watakuwa wakiagiza nyama kutoka ng’ambo na kuwauzia Wakenya,” Bw Musyoka akaeleza.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga