Habari za Kitaifa

Kalonzo alalamikia Raila na Ruto kuhusu mchakato wa kuunda upya IEBC

Na BENSON MATHEKA March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amemtaka Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kujumuisha upinzani katika mchakato wa kuunda upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Katika barua aliyowaandikia Ruto na Raila na iliyotolewa Ijumaa, Machi 28, Bw Musyoka aliwahimiza washirikishe upinzani katika majadiliano ya maana ili kuimarisha imani ya umma kwa IEBC na kuhakikisha mchakato huo ni wa haki na jumuishi.

“Ninaamini kwa dhati kuwa vyama; United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM), ambavyo sasa vimeungana upande mmoja, vinapaswa kushiriki mazungumzo nasi tulio upande wa upinzani ili kuhakikisha mchakato wa usawa na ujumuishi,” ilisema barua ya Bw Kalonzo.

Alisema msimamo wake unatokana na hitaji la kutimiza uwajibikaji.

“Msimamo huu umejikita katika misingi ya uwajibikaji, utawala bora, na sera madhubuti za umma.”

Kulingana na Kalonzo, kushindwa kushirikisha upinzani kutasababisha maamuzi yanayonufaisha UDA na ODM pekee, jambo ambalo litawafanya Wakenya kupoteza imani na IEBC.

Aliwataka Ruto na Raila wajifunze kutokana na historia na kulenga hatua zitakazohakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki, wa kuaminika, na unaoweza kuthibitishwa.

“Ninawaandikia kuhusu suala la kitaifa lenye umuhimu na dharura. Tunapojiandaa kwa uchaguzi ujao, ni muhimu sana kwamba kwa nia njema kabisa, tujifunze kutoka kwa historia yetu na kuweka kipaumbele hatua na taratibu zitakazohakikisha uchaguzi huru na wa haki, wa kuaminika na unaoweza kuthibitishwa,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Alionya kuwa ikiwa upinzani hautajumuishwa katika uamuzi huo, itakuwa ni kurudia makosa ya zamani yaliyosababisha migogoro ya uchaguzi na machafuko baada ya uchaguzi wa 2007|08.

“Aina hii ya siasa inahatarisha uthabiti wa taifa, inahujumu ustawi wa wananchi wa Kenya, na inaweka kwenye mizani umoja wa kitaifa na uhalali wa taifa letu,” aliongeza.