Kalonzo, Eugene, Omtatah wakejeli ndoa ya kisiasa ya Raila na Ruto
KIONGOZI wa Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka, aliyekuwa waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa na Mwanaharakati Okiya Omatatah wametaja mkataba kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kama ‘usaliti’ wa hali ya juu zaidi wa mamilioni ya Wakenya kote nchini.
Viongozi hao waliokuwa wakizungumza katika Tamasha la Mdahalo wa Watu jijini Nairobi jana, walitoa wito kwa Wakenya hasa vijana kuungana na kuwaondoa Bw Odinga na Dkt Ruto kwa kushinikiza maslahi ya kibinafsi.
Bw Musyoka aliahidi kuwaongoza Wakenya kupinga mkataba huo na kupigania mabadiliko katika serikali kwa kuleta mageuzi kama vile kuondoa ushuru wa nyumba.
‘Walidhani kuwa ni watu wachache tu wanaoweza kuongoza maandamano nchini. Wote wamekosea. Ninataka kutangaza kwamba kuanzia sasa na kuendelea, tutakuwa upinzani mwaminifu wa watu ambao unalenga kukomboa nchi hii. Ninawaomba vijana kusimama nasi katika safari hii ya kuwajibisha Rais Ruto na mshirika wake kwa ukiukaji wa haki za binadamu na hali inayozidi kuwa mbaya ya kiuchumi,” Bw Musyoka aliambia vijana waliokuwa wamekusanyika katika bustani ya Uhuru Park.
Pia alimkashifu Rais Ruto kwa kile alichokiita ushuru wa kidhalimu ambao umeharibu mazingira ya biashara na kuwafanya wawekezaji kuhamia nchi jirani.
“Iwe kuna handisheki au hakuna handisheki, ukweli ni kwamba lazima Rais Ruto aende. Msidanganywe kwamba watawapeleka nje ya nchi kupata kazi. Kampuni ambazo zilikuwa zitoe fursa hapa Kenya zimeondoka kwenda nchi jirani kama Tanzania. Ikiwa hawataleta fomula ya kufidia familia na wale waliouawa wakati wa maandamano basi hakuna kinachotoka KICC. Ni usaliti tu,” aliongeza akirejelea mkataba wa Raila na Ruto uliotiwa saini jana.
Kiongozi wa Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-Kenya) Eugene Wamalwa aliyeandamana na Bw Musyoka pia alishutumu waliohudhuria hafla hiyo katika KICC.
“Leo ni siku ya kihistoria. Ni siku ya kuchagua ikiwa unahitaji kusimama na wale ambao wako KICC ili kuwamaliza Wakenya au kusimama na watu wa Wakenya. Kama upinzani, tutasimama na Wakenya kuwakomboa. Nchi iko katika hali ya kusikitisha. Hakuna fedha kwa vyuo vikuu, shule na SHIF imefeli Wakenya. Vijana wanateseka na tutasimama nao,” alisema.
Seneta wa Busia Okiya Omtatah ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema waliokuwa KICC wana nia ya kuwatesa Wakenya kwa kuwatoza ushuru wa kidhalimu ili kufadhili malengo yao ya ubinafsi.
“Wanaokutana KICC ni wahalifu. Ni vyema wametuonyesha hulka zao mapema na kuanzia sasa na kuendelea, tunatangaza kuwakomboa Wakenya. Wameungana kuiba rasilimali zetu za umma na si kitu kingine. Tunatoa wito kwa vijana kujiandikisha kama wapiga kura kuanzia wiki ijayo ili tukomboe nchi,” Bw Omtatah alisema.
Tamasha la Mdahalo wa Watu (PDF) ni tukio la kila mwaka linaloandaliwa na Kituo cha Demokrasia ya Vyama Vingi-Kenya (CMD-Kenya) ili kukuza mazungumzo jumuishi na ushiriki kuleta mageuzi kati ya viongozi, wananchi, taasisi za serikali, mashirika ya kiraia, na wadau wa sekta ya kibinafsi.
Vijana waliohudhuria hafla hiyo jijini Nairobi walitoa wito kwa vijana wenzao kujiandikisha kama wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Vijana pia walishiriki katika mijadala kuhusu matatizo yanayoikabili nchi kama vile rushwa, ubadhirifu wa rasilimali za umma, kodi na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.