Kanuni zaruhusu wasiochagua STEM kusoma Hisbati ya Kawaida Gredi 10
Wanafunzi wa Gredi 10 ambao hawatachagua Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) lakini watachagua kusoma Hisabati ya Kawaida wataruhusiwa kufanya hivyo kulingana na matokeo yao ya tathmini ya Sekondari Msingi.
Katibu wa Elimu ya Msingi, Profesa Julius Bitok, alisema kuwa wanafunzi hao watapewa nafasi ya kusoma Hisabati ya Kawaida iwapo wataonyesha uwezo kupitia matokeo yao ya awali.
Katika waraka uliotumwa kwa wakurugenzi wote wa elimu wa kanda, kaunti na kaunti-ndogo, Wizara ya Elimu ilieleza mfumo wa utekelezaji wa awamu inayofuata ya Elimu ya Kuzingatia Umilisi (CBE), ambayo ni ngazi ya nne ya elimu ya msingi baada ya Chekechea, Shule ya Msingi na Sekondari Msingi.
Mbali na masomo ya lazima, mwanafunzi atachagua masomo matatu zaidi. Profesa Bitok aliwashauri wanafunzi kuchukua angalau masomo mawili kutoka mkondo wa mtaala waliochagua.
“Hii ina maana kwamba mwanafunzi anaweza kuchukua masomo matatu kutoka mkondo wa mtaala aliouchagua au masomo mawili kutoka humo na somo moja kutoka mkondo mwingine,” alisema Prof Bitok.
Hata hivyo, alisema kuwa iwapo uchaguzi wa taaluma ya mwanafunzi unahitaji somo moja kutoka kila mkondo, basi ataruhusiwa kufanya hivyo.
“Uchaguzi wa masomo utaongozwa na taaluma anayotazamia mwanafunzi, uwezo wake, nia na haiba, kwa msaada wa viongozi wa shule ya upili. Orodha ya masomo yote yanayotolewa katika shule ya upili chini ya CBC imetolewa na Taasi ya Kitaifa ya Ukuzaji wa Mitaala (KICD),” alisema.
Serikali tayari imeanza maandalizi ya utekelezaji wa CBE katika Shule ya Upili, huku Wizara ya Elimu ikitoa miongozo kuhusu masomo yatakayofundishwa.
Masomo manne ya lazima yatakuwa ni Kiingereza, Kiswahili, Hisabati ya Kawaida/Hisabati ya Msingi na Somo la Huduma kwa Jamii (CSL).
“Ili kufafanua, wanafunzi wote watalazimika kusoma Kiingereza, Kiswahili na Huduma kwa Jamii (CSL). Wanafunzi watakaochagua STEM watasoma Hisabati ya Kawaida, ilhali wale wa mikondo mingine watasoma Hisabati ya Msingi,” alisema Prof Bitok.