Karua adai Ruto na Museveni wamesuka dili hatari
KIONGOZI wa Narc Kenya, Bi Martha Karua amemshutumu Rais William Ruto na wenzake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuunda ‘muungano hatari ‘ ili kuendeleza utekaji nyara na hata mauaji ya watu wasiokubaliana na tawala zao.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Jumapili, Bi Karua alieleza kusikitishwa kwake na kuchelewa kwa Chama cha Wanasheria nchini Uganda kumpa cheti cha muda ili kumwakilisha kiongozi wa upinzani Kizza Besigye na mshirika wake Obeid Lutale katika Mahakama ya Kivita jijini Kampala.
Wawili hao walitekwa nyara nchini Kenya mnamo Novemba 16 kabla ya uzinduzi wa kitabu cha Bi Karua, Against the Tide, na kupelekwa Uganda ambapo wanakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kijeshi.
“Tabia hii inakiuka katiba ya Kenya, katiba ya Uganda, mkataba wa Afrika Mashariki, kanuni ya utawala wa sheria, na sheria zote za kimataifa za haki za binadamu. Iwapo Uganda ilikuwa na lolote kuhusu Dkt Besigye na mwenzake, Bw Lutale, wangeanza mchakato wa kuwarejesha nyumbani,” Bi Karua alisema.
Alisema kuwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni hatawali Kenya na kwamba wanajeshi wake au maajenti wake wa usalama hawawezi kufanya kazi katika ardhi ya Kenya wapendavyo.
“Ni muungano hatari alionao na utawala wa Ruto na unakumbuka wakati Boniface Mwangi alipotekwa nyara, tulisema tuna taarifa za uhakika kuwa kikosi cha utekaji nyara nchini Kenya kilikuwa na watu wa nje ambao ni pamoja na Waganda, Warundi, wengine kutoka Congo, na Mwenyezi Mungu anajua nchi gani nyingine,”alisema.
Bi Karua alikuwa amedai kuwa vyanzo vya kuaminika vinaonyesha kuwa vikosi vya utekaji nyara vinavyojumuisha maafisa wa jeshi na polisi hasa kutoka kabila moja na wageni kutoka Burundi, Uganda na Congo ni sehemu ya vikosi vinavyoendesha utekaji nyara Kenya.
Serikali ya Kenya awali ilikanusha kuwepo kwa kikosi cha aina hiyo.Katika mahojiano yake na Taifa Jumapili Ijumaa, kiongozi huyo wa Narc Kenya alisema kuwa kuchelewa kumruhusu kufanya kazi nchini Uganda katika kesi ya Dkt Besigye ni kinyume cha kanuni za EAC ambazo zinakubali ushirikiano wa kikanda, ushirikiano wa kiuchumi, na kisiasa.
“Inasikitisha kwamba tangu nilipoomba cheti, bado sijapata, hasa wakati tunasema tunaelekea kwenye shirikisho lakini hatujawianisha sheria zetu na Mkataba wa Afrika Mashariki,” alisema.
Kiongozi huyo wa Narc Kenya aliongeza: “Ni kuhusu usafirishaji wa bidhaa na wafanyakazi, ni kuhusu watu kuja pamoja. Inakuwaje wanasheria ndani ya shirikisho, au ndani ya EAC, wasifanye kazi bila leseni mbili?”
Bi Karua alisema licha ya kutuma ombi lake kwa mujibu wa sheria za Uganda kupewa leseni maalum ya kufanya kazi ya kumwakilisha Dkt Besigye na Bw Lutale, lililopokelewa na kupigwa muhuri mnamo Novemba 27, bado hajapokea leseni.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA