Habari za Kitaifa

Karua amtaka Raila kuhalalisha ndoa yake ya kisiasa na Ruto

Na DAVID MUCHUI March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga na mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa 2022 Bi Martha Karua, walikabiliana Jumatano, Machi 26, 2025 kuhusu nafasi ya waziri mkuu huyo wa zamani katika serikali ya Rais William Ruto.

Bi Karua, ambaye ni kiongozi wa People’s Liberation Party (PLP), alimshauri Bw Odinga kufanya maamuzi sahihi kwa kurasmisha “ndoa ya kisiasa” na Rais Ruto.

Akiweka wazi kuwa wao bado ni marafiki, Bi Karua alisema walikubaliana kutokubaliana kuhusu ushirikiano wa ODM na serikali.

Wawili hao waligombea urais pamoja mwaka 2022 lakini hawakufanikiwa.

Bi Karua alisisitiza kuwa upinzani kuungana na serikali kunakiuka misingi ya Katiba na demokrasia.

“Ikiwa unachanganya wachache na walio wengi bungeni, unawanyima wananchi uwezo wa kukosoa serikali,” alisema, akiongeza kuwa msingi wa demokrasia ya vyama vingi ni kuwa na chama kikuu tawala na chama kikuu cha upinzani.

“Tunawabariki wanaoona ni sawa kujiunga na serikali ya mseto, lakini nawaomba waingie katika ndoa takatifu ya kisiasa kwa kusajili muungano wao kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa,” aliongeza.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/koma-kumkejeli-matiangi-wazee-wamuonya-raila/

Bi Karua aliyasema haya alipohudhuria mazishi ya Julius Murungi, mkwe wa Gavana wa Siaya, James Orengo, huko Chogoria, Kaunti ya Tharaka Nithi.

Mnamo Machi 7, 2025, Bw Odinga alitia saini Mkataba wa Makubaliano na Rais Ruto lakini akasisitiza kuwa haukuwa  mkataba wa muungano kati ya chama tawala cha UDA na ODM.

Bi Karua alisema kuwa ushirikiano wa kisiasa unaofuata sheria utatoa fursa kwa mijadala yenye afya katika siasa za taifa.

Kiongozi huyo wa PLP alisema ataendelea kusimama kidete kama mpinzani kwani ni haki yake kutofautiana na washirika wake wa zamani.

“Lazima tuendelee kuikosoa serikali, kuuliza maswali kuhusu sera zake, kupinga utekaji nyara, mauaji ya kiholela na uporaji wa fedha za umma. Lazima tuendelee kupinga mateso yanayosababishwa na SHIF,” aliongeza.

Hata hivyo, Bw Odinga alisisitiza kuwa hajaingia serikalini bali amepeana tu wataalamu kwa Rais Ruto.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/raila-kwa-gachagua-sitaki-unafiki-sitamuacha-ruto/

“Tunapinga ukabila, tunapinga ubaguzi katika ugavi wa raslimali za umma. Hatujaungana na Rais Ruto, bali ni yeye aliyetuomba msaada wakati alipokuwa kwenye presha,” alisema Bw Odinga.

Aliongeza, “Sijaingia serikalini na mimi si sehemu ya serikali.”

Akimtetea Bw Odinga, mshauri wa Rais William Ruto, Moses Kuria, alidai kuwa alijiunga na serikali ili kuokoa nchi.

“Wakati wa maandamano ya Gen Z, Bw Odinga angeweza kuchagua kuiacha nchi iangamie. Lazima tupinge ufisadi na utekaji nyara bila kujificha nyuma ya ukabila,” alisema Bw Kuria.

Bw Odinga aliandamana na Gavana wa Busia, Paul Otuoma.