Kaunti za Magharibi zilivyotumia zaidi ya Sh1 bilioni kwa safari
MDHIBITI wa Bajeti amekosoa matumizi ya Sh1.442 bilioni zilivyotumiwa na kaunti za Magharibi katika safari za humu nchini na mataifa ya kigeni ilhali zimeshindwa kufikia malengo yake ya kukusanya ushuru.
Hii ni kulingana na ripoti kuhusu bajeti ya 2023/2024.
Ripoti hiyo imeashiria kuwa kaunti nne za Magharibi, Bungoma, Busia, Kakamega na Vihiga, zilitumia jumla ya Sh1,367.81 bilioni kusafiri nchini katika kipindi cha hadi Juni 30, 2024.
Bungoma iliongoza kwa kutumia Sh419.79 milioni kusafiri nchini ikifuatiwa na Kakamega Sh406.01 milioni huku Busia na Vihiga zikitumia Sh250.16 milioni na Sh291.85 milioni kwa usafiri nchini mtawalia.
Serikali ya Kaunti ya Kakamega ilitumia Sh218.50 milioni kusafiri humu nchini huku Bunge la Kaunti likinyofoa Sh187.51 milioni kusafiri nchini.
Kwa safari za nje ya nchi, Serikali ya Kaunti ilitumia Sh8.21 milioni nalo bunge la kaunti likitumia Sh4.42 milioni.
Baadhi ya ziara za kigeni zilizohudhuriwa na maafisa wakuu wa Kaunti ya Kakamega ni pamoja na mkutano rasmi wa jamii ya Waluhya Amerika na kutazama michezo ya shule za sekondari nchini Rwanda.
Kakamega ilitumia Sh1,350,600 kuhudhuria mkutano wa jamii ya Waluhya na Sh570,680 kuhudhuria Mashindano ya Ubingwa ya Shule za Afrika Mashariki Muhula wa Pili FEASSSA, Rwanda.
Bungoma ilitumia kiasi cha Sh419 milioni kusafiri humu nchini ikiwemo Sh64.16 milioni zilizotumiwa na Bunge la Kaunti na Sh355.63 milioni za serikali ya kaunti.
Ziara nje ya nchi ziligharimu Sh6.16 milioni ikiwemo Sh1.26 milioni za bunge la kaunti na Sh4.91 milioni za serikali ya kaunti.
Kaunti hiyo iliandikisha matokeo duni huku ikimudu kukusanya Sh439.48 milioni ikilinganshwa na mapato yaliyotarajiwa ya Sh868.20.
Jumla ya Sh250.16 milioni zinazojumuisha Sh108.25 milioni zilizotumiwa na bunge la kaunti na Sh141.91 milioni za serikali ya kaunti zilitumika kugharamia usafiri Busia.
Vihiga ilitumia Sh291.85 milioni zinazojumuisha Sh118.49 milioni zilizotumiwa na bunge la kaunti na Sh173.36 milioni za serikali ya kaunti, katika kusafiri nje ya nchi.
Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale amemkashifu Gavana Fernandes Barasa kwa kutumia Sh418 milioni kusafiri licha ya matatizo ya kifedha yanayokabili kaunti.
“Hii inaibua maswali kuhusu fedha zinazopatiwa kipaumbele katika Kaunti ya Kakamega. Kaunti kama vile Kakamega zinazong’ang’ana kutatua changamoto zinazohusu miundomsingi, afya na elimu, kiwango hiki cha matumizi ya usafiri huenda kisiwape manufaa ya papo kwa hapo wakazi,” alisema Seneta Khalwale.