Kesi za kupinga kuondolewa kwa Gachagua zasukumwa Januari 2025
KESI zote za kupinga kuondolewa kwa Rigathi Gachagua kama Naibu wa Rais na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani Prof Kithure Kindiki zitasikizwa Januari 2025.
Majaji Eric Ogola, Antony Mrima, na Freda Mugambi waliahirisha kusikizwa kwa kesi zaidi ya 30 hadi Januari 23, 2025, ili kumruhusu Bw Gachagua kuendelea na rufaa ya kupinga uteuzi wa jopo lao kusikiliza kesi hizo.
Bw Gachagua anapinga hatua ya Naibu Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu kuwateua majaji kushughulikia kesi hizo.
Bw Gachagua na Bw Munyi Mathenge na walalamishi wengine waliteta kuwa uteuzi wa majaji hao watatu ulifanywa kinyume cha utaratibu kwa vile DCJ hana mamlaka kama hayo.
Walalamishi hao walishikilia kuwa uteuzi wa majaji kuamua masuala mazito ya kikatiba ni jukumu la Jaji Mkuu na naibu wake hana uwezo wa kisheria kuwateua majaji.
“Tunafahamu kwamba kuna pande zilizowasilisha rufaa kupinga uteuzi wa jopo hili,” walisema Majaji Ogola, Mrima, na Mugambi wakiahirisha kesi hizo.
Kabla ya kuahirisha kesi hizo, mawakili wa upande wa walalamishi wakiongozwa na wakili Dkt John Khaminwa, Danstan Omari, Kibe Mungai, Njiru Ndegwa na Sam Nyaberi walieleza kutoridhishwa na uamuzi wa Jaji Mkuu Martha Koome kuongoza hafla ya kuapishwa kwa Prof Kindiki kama Naibu Rais wa tatu, tangu kuzinduliwa kwa Katiba ya 2010.
Bw Omari alisema walilalamishi hawakufurahishwa na hatua hiyo na akasema haki haikutendeka.
Bunge la Kitaifa kupitia kwa mawakili Eric Gumbo na Peter Wanyama waliwatetea majaji hao wakisema pande ambazo hazikuridhika na uamuzi wa mahakama zinafaa kukata rufaa.
Majaji hao pia waliwaruhusu walalamishi wawili Dkt Clarence Eboso na Bi Wanjiru Mwangi kuondoa kesi zao za kupinga kuteuliwa kwa Prof Kindiki kama Naibu Rais.
Majaji wa Mahakama ya Rufaa Patrick Kiage, Aggrey Muchelule, na George Odunga mapema wiki hii walisema kwamba watasikiliza rufaa hiyo kabla ya Krismasi mwaka huu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA