Habari za Kitaifa

Kibarua kwa Ruto kupangua serikali yake ya ‘Wenye Hisa’ na kuunda jumuishi

Na MOSES NYAMORI, BENSON MATHEKA July 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto anakabiliwa na kibarua kusawazisha maslahi ya kisiasa, kuacha kumbukumbu, kuchaguliwa tena, kulazimishwa kuchagua wataalam na kuhakikisha usawa wa maeneo anapounda upya Baraza lake la Mawaziri.

Rais pia atajikuna kichwa kutimiza matakwa mengi ya vijana – ambayo ni pamoja na kuwateua wataalamu katika wizara- ili kupunguza kutoridhika kwao na maamuzi yake. Vijana hao wameandaa maandamano makubwa, na kumlazimisha Rais kufanya maamuzi ambayo hayajawahi kushuhudiwa, miongoni mwao kuondolewa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.

Utata unaomkumba Rais unatokana na kukumbatia upinzani katika uamuzi ambao unaweza kuhusisha baadhi ya washirika wa Raila Odinga katika utawala wake bila kuibua hisia za kisiasa, haswa kutoka kwa mrengo wa kisiasa wa naibu wake Rigathi Gachagua.

Tayari kuna mtafaruku kati ya Dkt Ruto na Bw Gachagua. Kuongezeka kwa mizozo kunaweza kumtatiza katika uchaguzi wa 2027 huku akijaribu kuzima wimbi linalotishia maisha yake ya kisiasa.

Baraza la Mawaziri lililovunjwa kwa kiasi kikubwa liliundwa na watu kutoka maeneo ambayo yalidhaniwa kuwa yalimpigia kura Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, wengi wao wakiwa wa Mlima Kenya na Bonde la Ufa.

Kwa kiasi kikubwa inatarajiwa kuwa Rais atatumia muda huo kushughulikia baadhi ya malalamishi kwamba uteuzi wake unafaidi maeneo hayo mawili hasa baada ya kutangaza mipango yake ya ‘mpangilio mpana wa kisiasa’ kuunda yenye ufanisi zaidi.

Naibu wake, Bw Gachagua, amewahi kukumbusha upinzani kwamba utawala wa Kenya Kwanza ulikuwa kama kampuni ya wenye hisa, na ni wale tu walioichagua wana hisa nyingi.

“Serikali hii ni kampuni ambayo ina hisa. Kuna wamiliki ambao wana hisa nyingi, na wale walio na chache tu, wakati wengine hawana kitu. Uliwekeza kwenye serikali hii na lazima uvune. Ulipanda, ulilima, uliweka mbolea na kunyunyuzia maji, na sasa ni wakati wa kuvuna,” Bw Gachagua alinukuliwa akisema mara kwa mara.

Waliokuwa mawaziri Kithure Kindiki (Mambo ya Ndani), Njuguna Ndung’u (Fedha), Zacharia Njeru (Maji), Moses Kuria (Utumishi wa Umma), Alice Wahome (Ardhi), Mithika Linturi (Kilimo) na Mwanasheria Mkuu Justin Muturi wote wanatoka eneo la Mlima Kenya. Kipchumba Murkomen (Barabara na Uchukuzi), Davis Chirchir (Nishati), Florence Bore (Ulinzi wa Kazi na Jamii) na Simon Chelugui (Ushirika na Biashara Ndogo na za Kati) wanatoka Rift Valley.

Matamshi ya Dkt Ruto ya kuwashirikisha wahusika wengine wa kisiasa haswa wa upinzani, yanamaanisha kuwa atalazimika kutoa mhanga baadhi ya washirika wake waliomsaidia kutwaa mamlaka ili kushughulikia maeneo mengine ya nchi na vilevile kutimiza matakwa ya vijana ambao wanataka Baraza la Mawaziri lenye uadilifu.

‘Nitashiriki mara moja katika mashauriano ya kina ya sekta mbalimbali na mirengo ya kisiasa, kwa lengo la kuunda serikali pana ambayo itanisaidia katika kuharakisha utekelezaji wa lazima, wa haraka wa mipango ya kukabiliana na madeni, kupanua nafasi za kazi, kuondoa ubadhirifu na mashirika mengi ya serikali na kuangamiza ufisadi na hivyo kuifanya serikali kuwa yenye ufanisi,” Rais alisema

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Bw Raila Odinga jana kiliashiria nia yao ya kushiriki mazungumzo kuhusu sura mpya ya serikali.