Habari za Kitaifa

Kilonzo Jnr afufua mpango wa matibabu ulioanzishwa na Gavana Kivutha

Na PIUS MAUNDU  March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HATUA ya Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior ya kufufua mpango wa matibabu unaohusishwa na mtangulizi wake Kivutha Kibwana imewafurahisha wakazi wanaokabiliana na huduma duni za afya.

Haya yanajiri wakati Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu amekashifu tabia ya magavana kutelekeza miradi ya mabilioni ya pesa inayohusishwa na watangulizi wao.

Bw Kilonzo Junior anadai mpango wa bima ya afya unaosimamiwa na serikali ya kitaifa umeshindwa kutoa huduma kwa wakazi wengi wa kaunti.

Ili kuimarisha Huduma ya Afya kwa Wote, Kaunti ya Makueni katika bajeti ya 2025/2026, gavana huyo amewaagiza wakazi kuutambua kama mradi unaofaa kupewa kipaumbele katika mpango wa sasa wa kuandaa bajeti.

“Maelezo yetu ni kwamba umma unapaswa kuwasilisha jambo hili kwa uwazi katika mikutano inayoendelea ya kushirikisha umma ili tutenge pesa kwa mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote Makueni. Tumekubaliana na madiwani na Bunge la Kaunti kwamba hili lipewe kipaumbele,” Bw Kilonzo Junior alisema alipokuwa akikagua miradi katika Wadi ya Tulimani Jumatano, Machi 26, 2025.

Chini ya mpango huo maarufu kama Kivutha Card, watu watafurahia huduma za afya bila malipo katika hospitali za umma za kaunti walizochagua baada ya kulipa Sh500 kwa mpango wa bima ya kijamii.

Kadi hiyo pia itatoa huduma za afya bila malipo kwa wazee.

Alipokuwa akifanya kampeni, kiongozi huyo ni miongoni mwa wanasiasa waliopuuzilia mbali mpango huo akisema hautegemewi.

Zaidi ya mwaka mmoja afisini, ameangazia sekta ya afya na hivyo kuzua kilio kikubwa kuhusu huduma duni za afya katika hospitali za umma za Makueni ambazo zina sifa ya uhaba wa dawa na bidhaa nyingine za matibabu.