Kindiki akiri utajiri wake umeongezeka tangu ateuliwe waziri 2022
ALIYEKUWA waziri wa usalama wa ndani, Profesa Kithure Kindiki, amekiri kuwa utajiri wake umeongezeka hadi Sh695 tangu alipochukua usukani.
Akipigwa msasa Alhamisi mbele ya Kamati Maalum, Profesa Kindiki alikanusha kuwa utajiri wake ambao umeongezeka kwa Sh150 milioni, umetokana na shughuli haramu.
“Jinsi nilivyosema nilipohojiwa mara ya kwanza, utajiri wangu ulikuwa Sh544 milioni kabla ya uteuzi wangu. Sasa umeongezeka hadi Sh694 milioni,” alisema Profesa Kindiki.
Alieleza Kamati hiyo ya Upigaji Msasa inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula kuwa, “sijanufaika kutokana na biashara yoyote haramu na sijawahi kufanya biashara yoyote na serikali.”
Aidha, Profesa Kindiki anayemiliki Shirika la Mawakili alikana kwamba utajiri wake umeongezeka kutokana na mshahara au malimbikizi aliyokuwa akipata kama waziri.
“Ingawa kwa sasa sihudumu kama wakili, shirika langu la Sheria lingali hai na linafanya kazi,” alisema.
“Mshahara wangu wote unatumika kulipa bili.”
Bw Kindiki vilevile alifichua kuwa deni alilolipwa mara tu alipoteuliwa kama waziri kwa mara ya kwanza, lilichangia kuongeza mali yake.
“Kuna ada zinazohusu huduma nilizotoa kama wakili. Baadhi ya malimbikizi ya ada hizo sikuwa nimelipwa lakini sasa nimelipwa. Miezi miwili tu baada ya kuteuliwa kama waziri wa usalama wa ndani, mteja wangu mmoja alinilipa kitita cha hela nilizokuwa namdai kwa huduma za kisheria nilizompa.”
Kando na Shirika lake la mawakili, Bw Kindiki alisema kuwa anamiliki biashara ndogondogo hapa na pale akisisitiza kuwa,” hakuna utajiri wangu umetokana na mshahara au malimbikizi.”
Kwa jumla, Bw Kindiki alisema mali yake inajumuisha majumba mawili yenye thamani ya Sh235 jijini Nairobi na Tharaka Nithi, magari yenye thamani ya Sh17 milioni, akiba katika mashirika ya sacco na mapato kutokana na shirika lake la mawakili.
Profesa Kindiki ameandikisha historia kama waziri wa kwanza nchini kupigwa msasa mara mbili kwa wadhifa uo huo katika serikali moja, kufuatia hatua ya Rais William Ruto kumfuta kazi na kisha kumteua kuhudumu katika baraza jipya.
Mawaziri wengine waliofutwa kazi baada ya Rais Ruto kulivunja baraza lake kabla ya kuwarejesha lakini katika wizara tofauti ni pamoja na aliyekuwa waziri wa ulinzi Aden Duale, aliyeteuliewa kumrithi Bi Soipan Tuya katika wizara ya mazingira.
Bi Soipan Tuya atakuwa Waziri mpya wa ulinzi iwapo uteuzi wake utaidhinishwa na Bunge.
Mawaziri wa zamani ikiwemo Bi Rebecca Miano, Alice Wahome, Kipchumba Murkomen na aliyekuwa nwanasheria mkuu Justin Muturi, vilevile walirejeshwa baada ya kufutwa kazi.