Habari za Kitaifa

Kindiki aliyekuwa kisiki kwa Gachagua, ‘amempokonya’ kazi ya unaibu rais

Na CHARLES WASONGA, BENSON MATHEKA October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NI rasmi sasa kwamba Profesa Kithure Kindiki ndiye atajaza nafasi ya Naibu Rais baada ya kuondolewa mamlakani kwa Bw Rigathi Gachagua.
Profesa Kindiki ambaye amekuwa akihudumu kama Waziri wa Usalama, aliteuliwa na Rais William Ruto Ijumaa Oktoba 18, 2024.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula katika kikao cha Ijumaa majira ya asubuhi.
“Nimepokea ujumbe kutoka kwa Mheshimiwa Rais William Ruto akimteua Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya baada ya nafasi hiyo kusalia wazi mshikilizi alipoondolewa afisini. Ujumbe huo kutoa kwa Rais umeandamanishwa na stakabadhi hitajika kuhusu mteule huyo,” Bw Wetang’ula akawaambia wabunge.
Bw Gachagua, ambaye amelazwa katika Hospitali Karen baada ya kuugua Alhamisi, alitimuliwa baada ya Bunge la Seneti kuidhinisha mashtaka  matano kati ya kumi na mmoja yaliyoorodheshwa katika hoja ya kumwondoa afisini.
Bw Gachagua alikabiliwa na mashtaka 11 yaliyojumuisha ukiukaji wa Katiba na sheria mbali mbali za nchi, utovu wa maadili na matumizi mabaya ya mamlaka.
Kwa sasa Prof Kindiki anahudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, jukumu ambalo ameshikilia tangu Oktoba 2022, akapumzishwa kati ya Julai 11, 2024 na Agosti 8, 2024, wakati Rais alipovunja Baraza lake la Mawaziri.
Akiwa Waziri wa Usalama  wa Ndani  na Utawala wa Taifa,  Prof Kindiki ameongoza na kusimamia mageuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na: Mpango wa Uboreshaji wa Vifaa vya Polisi kwa kiasi kikubwa kuimarisha uwezo wa huduma za usalama za Kenya; kukamilika kwa mfumo mkakati wa kuanza utekelezaji wa kuboresha Polisi yaliyopendekezwa na  jopo lililoongozwa na  Jaji mstaafu David Maraga na kuimarisha vita dhidi ya ujangili na ukosefu wa usalama kwa ujumla kote nchini miongoni mwa mafanikio mengine.