Habari za Kitaifa

Kitendawili cha mgonjwa kuuawa kwa kukatwa koo hospitali kuu ya Kenyatta

Na KAMORE MAINA February 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

POLISI  huko Kilimani wanachunguza mauaji ya mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Gilbert Kinyua, 39, alipatikana amefariki katika kitanda chake ndani ya Wadi 7B katika KNH Ijumaa asubuhi.

Koo lake lilikuwa limekatwa, kulingana na habari iliyotolewa kwa polisi na maafisa wa usalama wa hospitali hiyo.

Muuguzi ambaye alikuwa akifanya ukaguzi wa kawaida kwa wagonjwa, aligundua kisu kilichokuwa na damu kinachoaminika kuwa silaha ya mauaji.

Kisu kilikuwa kimeangushwa juu ya paa la orofa ya kwanza ya hospitali hiyo.

Kinyua alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo mnamo Desemba 11.

Makachero kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai Kilimani (DCI) walitembelea eneo la tukio na kupata kisu hicho.

Wapelelezi hao pia waliwahoji wagonjwa kadhaa kuhusu matukio ya usiku wa mauaji hayo.

Mgonjwa mmoja aliwaambia wachunguzi kwamba kulikuwa na ghasia katika wadi iliyo karibu saa sita usiku. Hata hivyo, hakuna mgonjwa hata mmoja katika wadi  hiyo aliyemwona mshambuliaji huyo.

Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi Michael Muchiri alisema kuwa maafisa wa DCI wa Kilimani tayari wamechukua hatua.

Chanzo kinachofahamu uchunguzi huo kiliambia Taifa Leo kwamba DCI bado haijapata picha za CCTV kusaidia uchunguzi, kwani kamera za usalama hazikuwa zikifanya kazi wakati wa tukio.

Katika taarifa, wasimamizi wa KNH walithibitisha kisa hicho, na kusema hospitali hiyo ilikuwa ikishirikiana na polisi kutegua mauaji hayo.

“Hospitali inashirikiana kwa ukaribu na mamlaka za kutekeleza sheria na imeanzisha uchunguzi wa ndani ili kuhusiana na tukio hilo,” ilisema taarifa ya kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt W.K. Sigilai.

Dkt Sigilai aliongeza, “KNH imejitolea kutoa mazingira  salama kwa wote.”

Alisisitiza kwamba usalama na ustawi wa wagonjwa, wafanyikazi, na wageni ni “kipaumbele kikuu” cha hospitali.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA