Habari za Kitaifa

Koma kumkejeli Matiang’i, wazee wamuonya Raila

Na WYCLIFFE NYABERI March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wazee kutoka Kaunti ya Kisii wamejitokeza kutangaza kuwa wanaunga mkono azma ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Wazee hao, aidha wamedokeza kuwa Dkt Matiang’i atarejea humu nchini hivi karibuni kubuni mikakati zaidi ya kufaulisha azma yake inayolenga kumng’atua mamlakani Rais William Ruto na wakamtaka kiongozi wa chama cha ODM kukoma kumkejeli waziri huyo wa zamani.

Wakiongozwa na aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Kisii, Bw David Kombo, wazee hao wanaotoka ukoo wa Dkt Matiang’i walitaja mfano wa utendakazi mzuri wa waziri huyo alipokuwa akihudumu katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta kama dhihirisho anatosha kuwa rais.

Walisema ufanisi ulioafikiwa na Dkt Matiang’i katika wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), Elimu na Masuala ya Ndani ni sababu tosha za kiongozi huyo kupewa jukumu la kuliongoza taifa.

“Tuna imani Kenya haihitaji tu kiongozi mwenye maono bali pia mwenye ujuzi, mwadilifu na asiye fisadi. Dkt Matiang’i anazo sifa hizi. Kujitolea kwake katika utoaji wa huduma kwa raia na azma yake ya kuona Kenya yenye ufanisi, thabiti na yenye umoja si kitu cha kupingwa,” Bw Kombo alisema.

Wazee hao waliwakashifu viongozi kutoka jamii ya Abagusii waliokuwa wakitoa matamshi ya kupuzilia mbali azma ya Dkt Matiang’i wakiunga serikali ya sasa.

Licha ya kuegemea upande tofauti na wao, wazee hao waliwaambia wabunge hao kuuza sera za mwaniaji wao bila kujihusisha wala kulitamka jina la Dkt Matiang’i.

“Wacha wauze mtu wao kwa ustaarabu kwani Kenya ni nchi yenye demokrasia. Lakini kwetu sisi, tunampigia debe Dkt Matiang’i kuingia ikulu,” Bw Kombo aliongeza.

Mtaalamu mmoja wa elimu alisema ujio wa Dkt Matiang’i katika siasa za kitaifa unaibua kumbukumbu za aliyekuwa kigogo wa siasa za eneo hilo marehemu Simeon Nyachae.

“Mnakumbuka enzi za marehemu Simeon Nyachae? Alipokuwa akiwania kura za mwaka wa 2002 kupitia chama chake cha Ford People? Wabunge wote waliochaguliwa katika uchaguzi huo walikuwa wa chama chake. Hilo lilimsaidia kuwa na usemi katika serikali iliyoundwa wakati huo,” Bi Grace Mautia alisema.

Wazee hao walimtaka Bw Odinga kukoma kukejeli azma ya Dkt Matiang’i kuwania urais alipozuru kaunti ya Kisii wiki mbili zilizopita. Katika ziara hiyo, Bw Odinga aliulizwa na wanahabari ikiwa atamuunga Dkt Matiang’i katika ndoto yake ya kuingia ikulu mwaka wa 2027.

Swali hilo lilitokana na mtazamo wa wengi kuwa jamii ya Abagusii imemuunga Bw Odinga kwa miaka mingi katika safari zake nyingi zilizofeli za kuwania urais, na hivyo basi angefaa “kurudisha mkono”.

Akilijibu swali hilo, waziri huyo mkuu wa zamani alijibu kuwa Dkt Matiang’i hawezi kuchaguliwa rais wa Kenya kwa kura ya jamii yake pekee.Kauli hiyo iliwakera wafuasi wengi wa Dkt Matiang’i. Wengi waliichukulia kuwa hatua hiyo ilikuwa sawia na kupuuzilia mbali ndoto yake.

Kauli hiyo ilimzulia Bw Odinga kelele alipozuru kaunti ya Kisii siku chache baada ya kutia saini mkataba wa kisiasa na Rais Ruto. kwani vijana wenye hamaki walimzomea alipofika uwanjani Gusii kwa hafla ya timu ya Shabana.

“Waziri mkuu wa zamani ni mtu tunayemheshimu na tunampenda sana. Lakini ikiwa hana mpango wa kumuunga mkono mmoja kutoka jamii yetu, basi tunamuomba akome kumzungumzia,” Bw Kombo alisema.