Komesheni vita na ugomvi, Uhuru ahimiza anapoadhimisha bathidei yake ya 63
RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kudumisha amani na upendo licha ya changamoto nyingi zinazowakumba nyakati kama hizi
Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Milele FM Jumamosi Oktoba 26, 2024 anapoadhimisha miaka 63 tangu kuzaliwa kwake, Bw Kenyatta alisema umoja miongoni mwa Wakenya ni hitaji muhimu litakalohakikisha Kenya inasonga mbele na kustawi kiuchumi.
“Nyakati hizi siongei mengi. Nataka tu kuwahimiza Wakenya kuishi kwa amani na umoja. Tutambue kuwa sote tu binadamu na kwamba tuko na mapungufu ya hapa na pale,” rais mstaafu akaeleza.
“Tukomeshe vita na ugomvi. Tuendelee kupendana na tuungane kama Wakenya,” Bw Kenyatta akakariri.
Rais mstaafu alisema hayo wakati ya joto la siasa lilipanda nchini kabla na baada ya kupitishwa kwa hoja ya kumtimua afisini aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hoja ya kumwondoa mamlakani Gachagua ilipitishwa katika Bunge la Kitaifa mnamo Oktoba 8, 2024 baada ya kuungwa mkono na jumla ya wabunge 282 huku 44 wakiipinga.
Aidha, mnamo Alhamisi Oktoba 17, 2024 hoja hiyo iliidhinishwa katika Seneti baadhi ya maseneta kukubaliana na makosa matano kati ya 11 yaliyokuwa kwenye hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Bw Kenyatta alisema asingejumuika na familia na marafiki kusherehekea miaka 63 tangu kuzaliwa kwamba kwa sababu anahudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika kuhusu Amani jiji Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.
Mkutano huo ulioanza Oktoba 25, umewaleta pamoja viongozi wakuu wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Wawakilishi Maalum, Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda na mabalozi wa mataifa ya ulimwengu kwa ajili ya kujadili mikakati ya kusuluhsha mapigano na kudumisha amani Afrika.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Bw Kenyatta kuonekana hadharani kwa tangu Juni mwaka huu. Kutoonekana kwa kiongozi huyo kuliibua uvumi kuhusu hali yake ya kiafya.
Hii ndio maana mnamo Alhamisi Oktoba 24, kitengo chake cha mawasiliano kiliweka mitandaoni picha zake akiwasili nchini Côte d’Ivoire, akiwa buheri wa afya.