Habari za Kitaifa

Kumbatieni teknolojia ya kisasa mjiajiri, wanachuo waambiwa

Na LAWRENCE ONGARO September 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAMPUNI ya Microsoft imeanzisha mpango unaolenga kuimarisha ujuzi wa wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia mafunzo katika uwanja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

Mkurugenzi wa kampuni hiyo anayesimamia kitengo cha teknolojia katika ukanda wa Afrika Irene Githinji, amesema maafisa wao wameanza kuzuru vyuo vikuu nchini ili kuzihamasisha kuhusu umuhimu wa wanafunzi kupata mafunzo ya kiteknolojia.

Katika ziara ya maafisa wa Microsoft ya hivi majuzi katika bewa kuu la Chuo Kikuu cha Zetech, lililoko Mang’u, Kiambu, waliwahamasisha wanafunzi kuhusu kuhusu umuhimu wa mafunzo ya ICT katika maisha ya uchumi wa ulimwengu kwa ujumla.

“Chini ya mpango huu, wanafunzi watapewa mafunzo ya muda wa miezi mitatu mfululizo ili wapate ufahamu ufaafu katika ICT,” akasema Bi Githinji.

Alisema kampuni hiyo ina nafasi tele za ajira kwa wale watakaohitimu.

“Kwa wakati huu tunashirikiana na vyuo vikuu kadha ambapo tungetamani kuwapa mafunzo kamili na kuwapa ajira hapo baadaye,” Bi Githinji akaongeza.

Afisa huyo alisema kizazi kijacho kitakuwa cha wale wenye ujuzi katika nyanja za teknolojia ya habari na mawasiliano na ubunifu.

Mhadhiri wa idara ya ICT na mafunzo ya kiufundi katika Chuo Kikuu cha Zetech, Dkt Wilfred Gikaru aliwahimiza wanafunzi kutilia maanani masuala ya kiteknolojia kwa sababu huo ñdio mwelekeo wa kizazi kijacho.

Alisema wamekuwa na ushirikiano na kampuni ya Microsoft ili waweze kuwafunza wanafunzi masomo ya kiteknolojia na ubunifu.

Dkt Gikaru aliwashauri wajiandae kubuni ajira wao wenyewe ili kujiendeleza.