Kumbatieni vyama vya ushirika kulinda uchumi, ashauri Mudavadi
Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, ameonya kuwa uchumi wa Kenya bado uko hatarini kupoteza mtaji kutokana na migogoro ya kisiasa iwapo hautakikwa katika uwekaji akiba kupitia vyama vya ushirika.
Vyama vya ushirika, alisema, vinatoa njia endelevu na jumuishi ya kuunda utajiri, hasa kwa jamii ambazo kwa kawaida hazijajumuishwa katika mifumo rasmi ya fedha. Kenya ikiwa ni taifa linaloongoza Afrika katika vyama vya ushirika, kuna fursa ya kujenga uchumi imara unaotokana na akiba za ndani.
“Akiba ni msingi wa ukuaji wa uchumi. Lazima tuiendeleze kwa sababu bila akiba, nchi haiwezi kukua,” alisema wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya Ushirika ya103 jijini Nairobi.
Mudavadi alisema kutegemea harambee ni njia isiyoweza kutegemewa na vyama vya ushirika ni njia ya kuweka fedha ya kuaminika na jumuishi zaidi.
Alionya kwamba bila akiba thabiti za ndani, nchi itaendelea kuwa katika hatari.
“Tufanye vyama vya ushirika kuwa njia ya maisha. Viwe kama dini ya kiuchumi. Viwe vya kujenga uchumi wetu. Hivyo ndivyo tunavyoweza kuimarisha vyama vya ushirika. Nyote mnajua mnapigiwa simu mara kwa mara kwenda kwenye harambee,” alisema.
Aliongeza kuwa msingi imara wa vyama vya ushirika unaweza kulinda nchi wakati wa changamoto kama za kisiasa.
“Tukiwa na vyama vya ushirika imara, uchumi wetu utaimarika kwa sababu hata wakati wa matatizo ya kisiasa, mtaji hautatoweka. Hivyo ndivyo uchumi wa Kenya unavyoweza kuwa imara. Mara nyingine uwekezaji wa nje unaweza kuwa hatari,” alisema.
Kwa kuzingatia malengo ya kifedha ya pamoja, vyama vya ushirika huwaleta pamoja watu kutoka asili na maeneo tofauti. Katika maeneo kama hayo, kabila halina maana, kilicho muhimu ni uanachama, imani, na uwajibikaji wa pamoja.
“Tumejitolea kuanzisha sekta imara, yenye uwazi na uwajibikaji,” alisema.
Waziri wa Vyama vya Ushirika, Wycliffe Oparanya aliwahimiza washirika wa maendeleo kuacha kupeleka fedha kwa biashara ndogo kupitia benki za kibiashara na badala yake kutumia vyama vya akiba na mikopo, akisema zina ufanisi zaidi na ziko karibu na jamii.
Oparanya alisema fedha nyingi za misaada kwa biashara ndogo bado zinaingia benki licha ya vyama vya akiba na mikopo kuonyesha uwezo bora wa kuchukua mikopo na kulipa.
“Sacco zimekusanya Sh1.2 trilioni kupitia uwekaji akiba na kutoa Sh1 trilioni kwa mikopo huku Sh200 bilioni zikiwa bado hazijatumiwa. Hii inaonyesha hazina tu uthabiti bali pia zinafikia Wakenya wa kawaida zaidi ikilinganishwa na benki,” alisema.
Vyama vya ushirika vina nafasi muhimu katika mkakati wa serikali hasa katika mfumo wa thamani wa kilimo kama kahawa, maziwa na pamba.
Oparanya pia alifichua serikali kwa msaada wa Benki ya Dunia imeanzisha mfano wa vyama vya ushirika vinavyolenga jamii za vijijini pamoja na hazina ya kuzunguka ya Sh4.5 bilioni kusaidia wakulima.
Pia alitangaza kwamba Mswada wa Vyama vya Ushirika 2024 utawasilishwa hivi karibuni ili kushughulikia mapungufu ya utawala na kufafanua majukumu kati ya serikali za kitaifa na kaunti.