Kumbe mambo bado! Nchi yakwama tena sababu ya maandamano
VIJANA wa Gen Z walirejelea maandamano katika miji kadhaa nchini kuelezea kutoridhishwa kwao na mikakati iliyotangazwa na Rais William Ruto kutimiza matakwa yao, ikiwemo kuwafuta kazi mawaziri wake.
Walijtokeza katika miji ya kaunti 40 kwa maandamano kumshinikiza Rais aondoke mamlakani wakisema wamepoteza imani na utawala wake.
Yalikuwa maandamano ya pili makubwa tangu walipovamia Bunge mwezi jana kulalamikia kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 ambao Rais Ruto alikataa kutia saini.
Rais pia alikubali takwa lao na kutia saini mswada wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kufuta mawaziri, lakini hakuzima hasira zao hata baada ya kulaumu mashirika ya kigeni kwa kufadhili uasi dhidi ya serikali yake.
Katikati mwa miji mingi, kuanzia Nairobi, shughuli za kawaida zilitatizwa huku biashara zikifungwa polisi walipopambana vijana hao, kwa vitoa machozi mchana kutwa.
Licha ya baadhi yao kuuawa, kulemazwa, na kukamatwa kwa kuandamana, vijana hao walijitokeza kwa ukakamavu kuandamana.
Jana, baadhi walikamatwa pia, kupigwa risasi na kujeruhiwa lakini wenzao hawakuacha kuandamana.
Vikosi mbalimbali vya usalama viliweka ulinzi mkali katika majengo ya Bunge, Mahakama ya Juu na maeneo mengine ya serikali kuzuia kuvamiwa na waandamanaji ilivyofanyika mwezi jana, Juni 25.
Biashara zilifungwa Jumanne katika miji la Mombasa, Nairobi, Kisumu, Nakuru, Nyeri, Embu, Machakos, Makueni, Kajiado, Kericho, Eldoret, Nairobi, Uasin Gishu, Kakamega, Bungoma, Trans Nzoia, Homa Bay, Kisii, Meru, Laikipia, Baringo, Turkana na Kilifi miongoni mwa nyingine.
Barabara kuu nchini zilifungwa na waandamanaji na kukatiza shughuli za uchukuzi.
Katika mji wa Kitengela, kaunti ya Kajiado waandamanaji walifunga barabara yenye shughuli nyingi ya Namanga na kulazimisha barabara kadhaa kufungwa.
Waandamanaji hao waliongozwa na mwenyekiti wa vuguvugu la Free Kenya Bod Njagi ambaye alikuwa amebeba bendera ya Kenya.
Awali, mwendo wa saa mbili za asubuhi, walikongamana katika kituo cha magari ya uchukuzi cha Kitengela na kuhanganisha wenye magari.
Wananchi walilazimishwa kubeba matawi kuashiria kuwaunga mkono waandamanaji.
“Tunataka mabadiliko nchini. Wanasiasa wamekuwa wakitupuuza kwa muda mrefu. Kuanzia sasa, hali haitakuwa shwari nchini,” akasema kijana mmoja akiandamana na mbwa wake katika maandamano hayo.
Matrela kadhaa ambayo husafirisha bidhaa kutoka mji wa mpakani wa Namanga yalilazimika kusitisha safari.
Katika kaunti ya Trans Nzoia, afisi za serikali ya kaunti zilipewa ulinzi mkali na maafisa wa polisi walioshika doria mchana kutwa nje ya Town Hall Complex ambako kuna afisi ya Gavana George Natembeya.
Polisi jijini Mombasa walikabiliana na vijana waliojipenyeza miongoni mwa waandamanaji wa amani, na kusababisha vurugu katikati mwa jiji la Mombasa.
Maandamano hayo yalianzia maeneo ya Bombolulu ambako vijana walichoma magurudumu na kufunga barabara kabla ya polisi kufika huko na kuzima moto.
Maandamano hayo yalibadilika ghafla na ikamlazimu afisa mkuu kituo cha polisi cha katikati mwa jiji Bw Maxwell Agoro, kuwaomba waandamanaji kusitisha maandamano katika eneo la Sabasaba.
Waandamanaji halali waliondoka na polisi wakaanza makabiliano na vijana waliokuwa wakiwarushia mawe, kufunga barabara na kumwaga taka barabarani.
Vijana waliojaribu kufanya maandamano Kitale mjini walitawanywa na maafisa wa usalama katika kaunti ya Trans Nzoia.
Viwanda pia vilifungwa kote nchini kwa hofu ya kushambuliwa na waandamanaji.
Kulikuwa na maandamano katika kaunti kadhaa za eneo la Mlima Kenya, ngome ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, huku vijana wakimiminika barabarani kupinga serikali.
Bw Gachagua amekuwa akiwasihi vijana kutoandamana hasa baada ya Rais William Ruto kukataa kutia saini Mswada wa Fedha na kuvunja baraza lake la mawaziri.
Katika mji wa Karatina, Kaunti ya Nyeri, waandamanaji walipigana na polisi huku maandamano ya kuipinga serikali yakishika kasi.
Wakati mmoja, polisi walivamia soko la wazi la Karatina na kurusha vitoa machozi wakiwafuata waandamanaji.
Wafanyabiashara walipata hasara kubwa huku bidhaa zao zikiharibiwa katika mkanyagano uliofuata.
Biashara zingine zilifungwa kwa haraka kwa kuogopa uporaji.
Katika mji wa Nyeri, polisi waliweka vizuizi kwenye barabara kuu zinazoelekea vyuo vikuu vilivyo karibu.
Watu wanne walikamatwa nje ya bustani ya Whispers ambapo waandamanaji walipaswa kukutana ili kuanza maandamano yao.
Wanne hao walikuwa wameanza kuimba nyimbo za kuipinga serikali huku wakisubiri umati wa watu kuongezeka.
Katika mji wa Embu, waandamanaji wengi wanaoipinga serikali waliingia barabarani na kulemaza biashara katika mji huo na viunga vyake.
Waliandamana kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu. Kwa kuogopa uporaji, wafanyabiashara walifunga maduka yao haraka. “Ruto lazima aende! Ruto lazima aende!” walipiga kelele.
Katika mji wa Nanyuki, polisi wa Kaunti ya Laikipia walirusha vitoa machozi kutawanya kundi la vijana waandamanaji, baadhi yao walipoanza kuimba “Ruto Must Go”.
“Siogopi kusema Ruto Must Go, thubutu kunifyatulia risasi sasa,” mmoja wa waandamanaji aliwafokea maafisa wa polisi huku akiweka wazi kifua chake.
Katika mji wa Meru, maandamano hayo yalitekwa nyara na wanasiasa huku waandamanaji wanaomuunga mkono gavana Kawira Mwangaza wakiandamana nje ya Bunge la Kaunti ya Meru.
Haya yanajiri kabla ya pendekezo la kumuondoa madarakani kupangwa.
Katika mji wa Garissa, ulinzi mkali ulizuia vijana kujiunga na maandamano ya Jumanne.
Ripoti za Charles Wasonga, Sammy Kimatu, Kelvin Cheruyot, Stanley Ngotho, Titus Ominde, Sammy Lutta, Evans Jaola, Mercy Mwende, Mwangi Ndirangu, George Munene, David Muchui na Stephen Munene