Kuppet yataka marupurupu mapya kufidia walimu wanaposimama wakifundisha darasani
CHAMA cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) sasa kinapendekeza kuanzishwa kwa marupurupu ya ‘kusimama’ kufidia saa au muda walimu husimama madarasani kufundisha.
Aidha, Katibu Mkuu Akelo Misori anasema kuwa wanapendekeza nyongeza ya mishahara ya katika ya asilimia 30 na 70 chama hicho kinapoandaa mkataba wa maelewano (CBA) wa kati ya 2025 na 2029.
Katibu huyo anasema kuwa, katika kazi yao, walimu wanakumbwa na hatari nyingi za kiafya na hivyo wanahitaji kufidiwa.
“Baadhi ya walimu hufanya kazi kwa kati ya vipindi vitano na sita kwa siku, hali inayowasababishia matatizo katika viungo vya mwili na uchovu wa kiakili,” akasema katika mkutano mkuu wa Kuppet, tawi la Kisumu.
Mkutano huo ulifanywa katika shule ya Nyamasaria Comprehensive School, eneo bunge la Kisumu Mashariki. Bw Misori alisema Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) imeagiza Kuppet kuwasilisha taarifa yenye matakwa wanayotaka yashughulikiwe katika CBA ya 2025-2029.
“Nyongeza ya mishahara ya kati ya asilimia 30 na asilimia 70 ni takwa letu kuu. Walimu walioko katika gredi za chini za ajira wanafaa kupewa kiwango kikubwa cha nyongeza ikilinganishwa na walimu wakuu na wakuu wa Idara wanaopokea kiwango kikubwa cha mishahara,” akasema.
Kuppet pia itataka kuwa TSC ilipe marupurupu ya kufanyakazi katika mazingira hatari kwa walimu wa sayansi, usawazishaji wa marupurupu ya nyumba, nyongeza ya marupurupu ya usafiri yaliyofanyiwa marekebisho wakati wa mgomo wa walimu 2013.
“Kiwango cha sasa cha marupurupu ya usafiri kinaweza tu kumfaa mwalimu kwa muda wa wiki moja kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta kulikochangia kuongezwa kwa nauli,” akasema.
Wakati huo huo, Kuppet imeshikilia kuwa wanachama wake watasusia usimamizi wa Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) unaoanza wiki ijayo hadi matakwa yao yatimizwe.
Bw Misori alisema siyo sawa kwa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kuwapa walimu viwango vya marupurupu vilivyotumika mwaka wa 1997 kwani uchumi wa nchi umedorora.
“Baraza hilo linafaa kukoma kuwatumia walimu kama watumwa na kuzingatia kwamba walimu wanapitia hali ngumu ya kiuchumi. Malipo wanayotoa ni finyu mno,” akasema.
Kulingana na viwango vya sasa vya malipo, walimu wakuu ambao ndio wasimamizi wa vituo vya mitihani hulipwa Sh500 kwa siku huku walimu wanaosimamia watahiniwa wanapofanya mitihani hupata Sh450 huku wanaosahihisha mitihani hulipwa marupurupu ya Sh150 kwa siku.
Kuppet imependekeza kuwa walimu walipwe Sh3,000 kwa kutoa usaidizi kwa watahiniwa, Sh3,500 kwa wasimamizi wa shughuli hiyo na Sh4,500, kila siku, kwa walimu wakuu ambao ni wasimamizi wa vituo vya kufanyia mitihani.