Kuria, Owalo na Itumbi wapewa minofu serikalini na Rais Ruto
RAIS William Ruto amewatuza mawaziri aliofuta kazi, Moses Kuria na Eliud Owalo, pamoja na bloga wake mashuhuri Dennis Itumbi.
Ijumaa, Rais Ruto alimteua aliyekuwa Waziri wa Watumishi wa Umma Bw Kuria kama Mshauri Mkuu kwenye Baraza lake la Ushauri wa Kiuchumi.
Naye aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Digitali Bw Owalo sasa ni Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Idara ya Utendakazi na Usimamizi.
Mwanablogu Itumbi ametunikiwa wadhifa wa Mkuu wa Mikakati Maalum na Uchumi wa Sanaa Bunifu.
Teuzi hizo zilitangazwa kupitia waraka uliotolewa na Mkuu wa Wafanyakazi Ikulu na Watumishi wa Umma, Bw Felix Koskei.
Alieleza kwamba teuzi hizo zinalenga kupiga jeki utekelezaji wa ajenda ya serikali ya kuinua uchumi wa wananchi kutoka tabaka la chini kwenda juu maarufu Bottom Up Economic Agenda (BETA).
Uteuzi wa Bw Owalo ni wa kiwango cha uwaziri na majukumu yake yatakuwa pamoja na “utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini mwafaka ya miradi ya serikali kuambatana na mpango wa BETA.”
“Ofisi hiyo pia itafuatilia utoaji huduma katika wizara, idara na mashirika ya serikali,” waraka huo ulieleza.
Uteuzi wa Bw Kuria, uliendelea, utapiga jeki utekelezaji wa mpango wa BETA katika Serikali Jumuishi ya sasa – iliyoundwa baada ya Rais Ruto kujumuisha mawaziri watano kutoka upinzani, hususan wane wakitoka chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Kinaya
Hata hivyo, uteuzi wa Bw Kuria unaonekana kwenda kinyume na ahadi ya Rais kupunguza idadi ya washauri wake kwa asilimia 50.
Mwezi Julai akijibu matakwa ya vijana wa kizazi cha Gen Z walioendesha maandamano kwa wiki kadha nchini, rais alisema: Idadi ya washauri serikalini itapungua kwa hadi asilimia 50 kuanzia sasa hivi.”
Bw Kuria atajiunga na kundi maarufu la washauri wa Rais linalojumuisha Dkt David Ndii, Henry Rotich, Monica Juma, Mohammed Hassan na Nancy Laibuni – ambao inakisiwa hulipwa mshahara wa jumla wa hadi Sh 1 bilioni.
Bw Owalo, Bw Kuria, Njuguna Ndung’u (Fedha), Ezekiel Machogu (Elimu), Aisha Jumwa (Jinsia, Utamaduni, Sanaa), Zachariah Njeru (Maji) na Mithika Linturi (Kilimo) waliangukiwa na shoka kufuatia maandamano yaliyokumba taifa kwa majuma kadha.