Kwa Sakaja, ni utendakazi bora utamwokoa asitimuliwe na madiwani
MBUNGE wa Makadara George Aladwa amemtaka Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kushughulikia matatizo ya wakazi wa jiji la Nairobi.
Haya yanajiri huku madai yakizuka baadhi ya madiwani wanapanga njama ya kuwasilisha hoja ya kumtia afisini.
Bw Aladwa mnamo Jumatatu alisema kuwa Bw Sakaja hafai kuwapuuza madiwani ambao wamekuwa wakifuatilia utendakazi wake na hadi sasa hawajaridhishwa na rekodi yake tangu achaguliwe.
Wakati ambapo kuna gumzo kuwa huenda Bw Sakaja akatimuliwa, mwenyewe amejitokeza na kusema hatahangaishwa na watu wachache ambao hawafurahii kazi yake.
“Apange nyumba yake kwa sababu kile tunataka kuona ni maendeleo na si hadithi au ahadi zisizotimizwa. Kaunti ya Nairobi na kubwa na tunataka maendeleo,” akasema Bw Aladwa.
Ili kujikinga Bw Sakaja amekuwa akiwavutia madiwani wa ODM ambao ndio wengi upande wake na wikendi hata alionekana nyumbani kwa Kinara wa Azimio Raila Odinga kule Bondo, Kaunti ya Siaya.
Kuonekana kwake na Raila kulifasiriwa kuwa juhudi za kumrai Bw Odinga atulize joto la kisiasa linalomkabili katika kaunti.
Bw Aladwa alisema kuwa anafahamu kuwa gavana alikutana na madiwani wa ODM mnamo Jumatatu ila kitakachomwokoa ni utendakazi wake kwa sababu raia ndio wana usemi wa mwisho.
“Sina habari kuhusu mkutano huo ila nimesikia analenga kutuliza madiwani ambao wanaonekana wamemchoka na wanataka kumtimua,” akasema Bw Aladwa ambaye ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi.
Wiki jana, Bw Sakaja pia alikutana na madiwani wa Kenya Kwanza ambapo inadaiwa aliwaomba washirikiane kuyatatua baadhi ya matatizo yanayowakabili wakazi jijini.
Bunge la Kaunti ya Nairobi vimerejelea vikao vyake Jumanne baada ya mapumziko ya kipindi kifupi.
Baadhi ya madiwani ambao ni wandani wa Bw Sakaja wameonya kuwa hawatakubali hoja yoyote ya kumtimua Gavana iwasilishwe