Habari za Kitaifa

Maafisa 10,000, wakiwemo KDF kudumisha usalama msimu wa sherehe

Na STEVE OTIENO December 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JUMLA ya maafisa 10,317 kutoka Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), Huduma ya Magereza ya Kenya, Huduma ya Wanyamapori ya Kenya na Huduma ya Misitu ya Kenya wametumwa kote nchini kudumisha usalama wa umma na kushughulikia ukiukaji wa sheria msimu wa sherehe za Krismasi na mwisho wa mwaka.

Kutokana na hali hiyo, hakutakuwa na mapumziko ya Krismasi kwa maafisa wa polisi, huku wale walio likizoni wakiamrishwa kurudi kwenye vituo vyao vya kazi ili kuhakikisha hakutakuwa na matukio yoyote ya uhalifu wakati wa likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Pia usalama utaimarishwa katika vituo vya kuingia na kutoka nchini, hoteli, maduka makubwa, fuo za umma na maeneo ya watalii pamoja na miundombinu muhimu na maeneo ya Biashara ya Kati ya miji mkuu nchini. Hali ya usalama pia itaimairisha katika maeneo ya ibada na kumbi za burudani.

Maafisa zaidi wa trafiki watatumwa barabarani kushughulikia wanaoendesha magari kiholela, magari yanayobeba kupita kiasi na magari yasiyo na leseni na kuhakikisha hakuna msongamano.

Hizi ni baadhi ya hatua zinazotekelezwa na serikali kote nchini ili kulinda maisha na mali katika msimu huu wa sherehe ambazo mara nyingi huambatana na ongezeko la matukio ya uhalifu na ajali za barabarani huku watu wengi wakisafiri kuashiria kufunga na kukaribisha mwaka.

Katibu wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa Dkt Raymond Omollo alisema kuwa kituo cha kushughulikia usalama kinachojumuisha mashirika mengi ya kitaifa kimeanzishwa katika kambi la jeshi la Lang’ata.

Kituo hiki kitasaidiana na kamati za usalama na kijasusi za kanda na kaunti ambazo pia zitaanzisha vituo vyao vya mashirika mengi ambavyo vitakuwa vinafanya kazi kwa saa 24 siku saba kwa wiki.

“Wakenya wanapaswa kutarajia kuona uwepo wa polisi zaidi kwa sababu tumesambaza vitengo maalum zaidi ikiwa ni pamoja na Kitengo cha Silaha Maalum cha wanawake pekee na maafisa wa siri pamoja na polisi wa kawaida ili kuimarisha doria na ufuatiliaji katika miji mikuu,” Dkt Omollo alisema.

Huduma ya Kitaifa ya Polisi pia imeagizwa kubuni operesheni za msimu wa sikukuu ili kuratibu shughuli za usalama katika kaunti zote pamoja na kushirikiana na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama kutekeleza sheria za trafiki kwa madereva.

Kulingana na Utafiti wa Uchumi wa 2024, takriban watu 4,324 walipoteza maisha katika barabara za Kenya mwaka wa 2023, idadi ambayo ilipungua kwa kiasi kikubwa kutoka vifo 4,690 vilivyorekodiwa mwaka wa 2022.

Wakati wa siku ya kuadhimisha siku ya kuwakumbuka waasiri wa ajali za barabarani mnamo Novemba NTSA ilisema idadi ya waliojeruhiwa kutokana na ajali za barabarani nchini ilikuwa zaidi ya 10,000.

Mamlaka ilisema kwamba kuwa ajali za barabarani nchini zimepoteza maisha ya watu 4,047 kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la watu 321 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023.

Ni hali inayotia wasiwasi ambayo Wizara ya Masuala ya Ndani inataka kupunguza wakati wa msimu wa sherehe mwaka huu.

“Kamati zote za Usalama za kanda na Kaunti kwa kushirikiana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi na KWS zitachukua hatua hakikisha usalama wa watalii wa ndani na wa kimataifa wanaotembelea vituo vya mapumziko katika Bahari ya Pwani na maeneo ya vivutio vya watalii, Mbuga za Kitaifa na Hifadhi za Wanyama,” Dkt Omollo. alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA