Maafisa wa NYS walalama kutolipwa kazi ya ujenzi wa shule
OPERESHENI ya usalama katika eneo la Bonde la Ufa inayofahamika kama Maliza Uhalifu, imeangaziwa baada ya kundi la maafisa wa Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) waliohusishwa kujenga shule kulalamikia kukosa kulipwa.
Vijana wasiopungua 50 wa NYS wanadai jumla ya Sh3 milioni ambazo ni malimbikizi ya marupurupu yao ya miezi minne.
Operesheni Maliza Uhalifu (OMU) ilizinduliwa 2013 kuangazia ukosefu wa usalama katika kaunti za Turkana, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Baringo, Laikipia na Samburu.
Iliongozwa na kikosi kinachojumuisha KDF, GSU, ASTU, polisi wa kawaida na NPRS.
Maafisa hao waliojumuishwa kwenye operesheni hiyo Februari 2023, wamelalamikia kukosa kulipwa na kuongezewa muda wa kandarasi kinyume na maafikiano.
Akizungumza na Taifa Leo, afisa mmoja kutoka Nakuru alifichua walihusishwa kwenye operesheni hiyo kama maafisa wenye ujuzi ili kusaidia jeshi la KDF katika ujenzi wa shule Baringo, kama sehemu ya kuzima shughuli za majangili eneo hilo na kuanzisha maendeleo.
Kundi la kwanza la makurutu wa NYS lilitumwa eneo hilo kutoa huduma mbalimbali ikiwemo waashi, fundi wa mifereji, kazi za stima na nyinginezo.
Afisa huyo alisema walistahili kufanya kazi kwa miezi mitatu kwa mkataba wa kulipwa marupurupu ya Sh15,000 kila mwezi.
“Tulikuwa bado tunasubiri kuelekea katika maeneo yetu ya mafunzo baada ya kukamilisha mitihani yetu tulipopokea jumbe kupitia simu na kutuagiza kurejea chuoni. Tulitumwa katika operesheni kaunti hiyo ambapo KDF ilikuwa inajenga shule,” alisema afisa huyo.
Waliporejea vituoni, afisa huyo alisema wahudumu wa NYS walikuwa wameitisha malipo ya Sh1,000 kila siku lakini maafisa wasimamizi wakawashawishi kuchukua nusu ya kiasi hicho.
Alidai walipokea malipo ya kwanza baada ya kufanya kazi kwa miezi miwili yaliyotumwa kwa pamoja katika akaunti zao za benki mtawalia.
Nakala zilizofikia Taifa Leo zinaonyesha maafisa hao walitumwa kujenga shule mbalimbali ikiwemo shule za msingi za Chesitet, Chepkesin, Kositei, Koloa, Kapindasum, Arabal, Pura, Mukutani, Sambalat, Lomelo, Chemoril na shule ya sekondari ya Kapedo.
Tuliwasiliana na KDF kuhusu suala hilo lakini wakajitenga na shutuma hizo wakidai hawawajibiki kwa malalamishi ya maafisa husika.