Majaribio manne ya kumkinga Gachagua yalivyofeli kortini ‘usulubisho’ ukikaribia
UWEZEKANO wa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuendelea kushikilia wadhifa wake sasa unaning’inia huku Bunge la Kitaifa likianza rasmi Jumanne (leo) mchakato wa kumbandua mamlakani.
Jumatatu, Bw Gachagua mwenyewe alionekana kukata tamaa na kusema kuwa iwapo itaamuliwa aende nyumbani basi yupo tayari kufanya hivyo.
Hiyo hiyo jana, kesi nne ziliwasilishwa kortini kuzuia kuwasilishwa kwa hoja ya kumbandua mamlakani lakini zote ziligonga mwamba.
“Iwapo itaamuliwa kuwa niendelee kufanya kazi basi nipo tayari. Ikiamuliwa kuwa niende nyumbani pia nipo tayari,” akasema Bw Gachagua baada ya kutamatisha ziara yake ya siku tatu kaunti za Mlima Kenya ambako ni ngome yake ya kisiasa.
Katika kile ambacho kilionekana kama kuwaaga wafuasi wake akiwa naibu rais, Bw Gachagua alisema kuwa mshikilizi yeyote wa wadhifa huo kama atatokea ukanda huo, basi anastahili kuungwa mkono badala ya kupigwa vita.
“Kilio changu kwa watu wa Mlima Kenya ni kuwa msalie na umoja wenu. Si mimi pekee yangu naweza kuwaongoza, kiongozi yeyote anaweza kufanya hivyo. Hata hivyo, kusalia serikalini kwa miaka mingi na kupata maendeleo, lazima muungane.
“Kuondolewa kwangu ni njia ya kuwagawanya. Wakazi wa Mlima Kenya watapata tabu sana ndiposa wanataka nitimuliwe. Nawaomba msalie na umoja wenu kwa sababu watakuwa wamefaulu kutugawanya,
“Siasa zetu na maendeleo zitaisha kama hatuna mamlaka, nguvu au ushawishi. Kama kutakuwa na kiongozi mwingine, msiruhusu Mlima Kenya ugawanyike,” akasema.
Hii leo, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula anatarajiwa kutangaza kuwa amepokea notisi ya hoja ya kumbandua Bw Gachagua mamlakani.
Naibu Kiongozi wa Wengi Owen Baya (Kilifi Kaskazini) ndiye mdhamini wa hoja hiyo na ataiwasilisha bungeni huku Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse akitarajiwa kuiunga mkono.
Bw Wetang’ula atatoa mwelekeo jinsi ambavyo mchakato mzima wa kumbandua Naibu Rais utakavyoendelezwa. Hoja hiyo inataja ukiukaji mkubwa wa katiba kama sababu kuu ya kumwondoa Bw Gachagua mamlakani.
Takwimu kutoka Bunge la Kitaifa zinaonyesha kuwa zaidi ya wabunge 300 wametia saini nakala ya hoja ya kumbandua Bw Gachagua afisini kufikia Alhamisi wiki jana wakati ambapo hoja hiyo ilipelekewa Bw Wetang’ula.
Kikatiba, theluthi moja ya wabunge wanahitaji kutia saini nakala ya hoja ya kumbandua naibu rais kabla ya kufikishwa kwa Spika. Idadi hiyo ni wabunge 117 kati ya 349.
Hata hivyo, ili kupitishwa lazima idadi hiyo iwe ni theluthi mbili ya wabunge 349 na maseneta 45. Jana, wabunge wengi hawakutaka kuzungumzia hadharani lakini Mbunge wa Aldai Maryanne Keitany alisema hoja hiyo ipo.
“Hoja iliwasilishiwa kwa Spika mnamo Alhamisi wiki jana na tunatarajia atangaze bungeni leo na mchakato utakaofuata,” akasema Bi Keitany.
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alikuwa amesema atadhamini hoja hiyo lakini wabunge wa Kenya Kwanza walionekana kutopendezwa na hilo wakisema mara nyingi huwa hayuko bungeni.
“Atafaulu aje kushughulikia suala hili zito la kumng’oa naibu rais?” akahoji mbunge mmoja wa Kenya Kwanza ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Hapo jana kesi nne zilizowasilishwa kumwokoa Bw Gachagua ziligonga mwamba majaji wakiamrisha zishughulikiwe wiki ijayo. Kesi ya kwanza iliwasilishwa na Caroline Wambui Mwangi katika Mahakama Kuu lakini Jaji Lawrence Mugambi akaamrisha akasema itajwe mnamo Oktoba 9.
Kesi nyingine iliwasilishwa na vuguvugu la Sheria Mtaani kupitia wakili Danstan Omari lakini Jaji Chacha Mwita akaamrisha pia itajwe Oktoba 9 na kutaka washtakiwa wawasilishe stakabadhi za kesi kwa Bunge la Kitaifa na Spika.
Juhudi za kumwokoa Bw Gachagua zilianza asubuhi kupitia kesi iliyowasilishwa na Seneta wa zamani wa Kakamega Cleophas Malala ila Jaji Bahati Mwamuye akakataa kusimamisha mchakato wa kumbandua Bw Gachagua.
Katika kesi ya nne, watu watano wakiongozwa na Obuli Namenya pia walifika kortini wakisema kutimuliwa kwa Bw Gachagua ni kinyume cha katiba kwa kuwa umma ambao ulimchagua haukushirikishwa.
Ripoti ya David Mwere, Sam Kiplagat na Richard Munguti