Makachero wanyaka mwanamume akifanya ‘karamu’ ya ngono na watoto wa miaka 13-17
MAKACHERO kutoka Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI) jijini Nakuru wametibua karamu ya ngono katika eneo la Naka Estate na kumkamata mfanyabiashara anayeaminika kuwahadaa wasichana wa shule kushiriki ngono.
Watoto wasichana, wenye umri wa miaka 13-17, walikamatwa na polisi katika tamasha hiyo wikendi, wakibugia pombe na kujamiiana kwa pamoja.
Kulingana na polisi, mwanamme huyo mwenye umri wa miaka 42 anashukiwa vilevile kuwanajisi watoto zaidi ya 20.
“Mshukiwa amekuwa akifanya kazi na watu wengine ambao bado hawajakamatwa, kuwahadaa wasichana wa shule kushiriki ngono kwa pamoja, ambapo hurekodi matukio hayo na kisha kuuza video hizo kwa kati ya Sh9500 na Sh10,000. Amekuwa akiwarekodi watoto kadhaa ambao wamezuru majengo hayo na kisha kuuza video,” alifichua Kamanda wa Polisi, Nakuru Mashariki, Mohammed Wako.
Mshukiwa pia anasemekana kuwatumia watoto wengine kuwalaghai wahasiriwa wake kwenda katika tamasha hizo.
“Mshukiwa amekuwa akiwatumia watoto wengine kuwahadaa wahasiriwa wake kujihusisha katika matukio hayo. Amekuwa akiwalipa wasichana wa shule ada ya Sh500 na kisha kuuza video aliyorekodi kwa kati ya Sh9500 na Sh10,000,” alisema mkuu wa polisi.
Baadhi ya watoto ambao ni wahasiriwa wa hila za mshukiwa, walihadaiwa kwenda nyumbani kwake ambapo walidungwa kinachoaminika kuwa dawa za usingizi, kabla ya kunajisiwa.
Polisi walisema mshukiwa alikiri makosa yake kwa wazazi wa wahasiriwa, alipofumaniwa nyumbani kwake Naka Estate, baada ya msichana (13) aliyetoweka kwa siku kadhaa, kufichua siri kuwa amenajisiwa.
Watoto wawili ambao wamekuwa wakimsaidia kupata wahasiriwa wake wanasemekana kuwaongoza wazazi wa msichana kwa nyumba ya mshukiwa, ambapo walimfumania na watoto wengine.
“Msichana, 13, alitoweka kwa muda na aliporejea nyumbani alifichua amenajisiwa. Wazazi waliwaarifu polisi waliowasili katika nyumba ya kukodisha na kumkamata mshukiwa,” alifichua Bw Wako.
“Wakiwa korokoroni, wasichana hao wawili walimpigia simu mshukiwa na kumfahamisha wamepata wasichana wengine. Tulimwekea mtego na kuwakamata. Kwa jumla, tuna watoto watano wasichana, watatu walikusudiwa kuwa wahasiriwa.”