Habari za Kitaifa

Makosa ya Kawira yanayowapandisha mori madiwani Meru

Na MARY WANGARI August 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA Kawira Mwangaza anayepigania afisi yake mbele ya Seneti kwa mara ya tatu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kimsingi yaliyowasilishwa dhidi yake na madiwani wa Bunge la Kaunti ya Meru.

Spika wa Seneti Amason Kingi Jumatatu alisoma mashtaka yanayomkabili Gavana wa Meru ambayo ni pamoja na kukiuka katiba na sheria nyinginezo, ukosefu wa nidhamu na matumizi mabaya ya afisi.

Kuhusu kukosa maadili, Bi Kawira anadaiwa kupotosha umma kimaksudi kwa kutoa habari za uongo kuwa Sh86,000,000 zilikusanywa kupitia nambari ya Paybill 247247 Akaunti 0400163917899, iliyobuniwa baada ya mauaji ya Daniel Muthiani almaarufu Sniper ilhali ni Sh286,516 pekee zilizokusanywa.

“Kitendo hicho kilikiuka sifa za kimaadili na kanuni zinazohitajika kwa maafisa wa umma kinyume na Kipengee 19 kuhusu Maadili ya Afisa wa Umma na Kipengee 29 kuhusu Uongozi na Uadilifu,” Seneti ilielezwa.

Isitoshe, Kawira anadaiwa kutumia vibaya afisi yake ikiwemo kuwalipa madaktari 161 Sh74,340,000, za ziada kama malimbikizi ya kushughulikia dharura na kutumia mfumo usio wa kidijitali kulipa mishahara.

Anadaiwa kuongeza mzigo wa mshahara kwa zaidi ya Sh500 milioni, karibu nusu ya mapato ya kila mwaka kwa kuajiri wafanyakazi 111 wa kibinafsi katika afisi ya gavana.

Ameshutumiwa kumlipa Kiambi Christus Manyara, afisa wa mawasiliano ya umma katika afisi ya gavana, mshahara kamili na marupurupu akiwa angali rumande licha ya kushtakiwa kuhusu mauaji.

Kuhusu ukiukaji wa katiba, mkuu huyo wa kaunti anadaiwa kwenda kinyume na Vipengee 58(4) na 59A vya Sheria kuhusu Serikali za Kaunti kwa “kufutilia mbali kwa njia haramu uteuzi wa CPA Virginia Kawira Miriti kama Katibu/mkurugenzi wa Bodi ya Watumishi wa Umma Kaunti ya Meru, pasipo kura isiyopungua asilimia 75 ya madiwani wote wa Bunge la Kaunti na kuingilia mamlaka ya Bunge la Kaunti.”

Anadaiwa kukiuka Kipengee 4 cha Sheria kuhusu Uteuzi wa Watumishi wa Umma (Uidhinishaji wa Bunge za Kaunti) kwa kukosa kuteua wenyekiti wa Bodi ya Mapato Meru, Shirika la Fedha Meru, Bodi ya Huduma ya Vijana Meru na Bodi ya Taasisi inayosimamia Uwekezaji na Maendeleo, hivyo kukosa kuendesha Bodi hizo au kuwateua wenyekiti hao bila kupigwa msasa au kuidhinishwa na Bunge la Kaunti.

“Maafisa hao wa bodi zilizotajwa wanaendelea kupata na kutumia fedha za umma bila wanachama wa bodi walioteuliwa kutekeleza ungalizi kuhusu sekretariati ya bodi ili kuhakikisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha hivyo kuhujumu utowaji huduma,” linahoji Bunge la Kaunti ya Meru katika nakala ya mashtaka iliyowasilishwa kwa Seneti.

Inadaiwa alikataa kutekeleza mapendekezo au maamuzi ya Bunge la Kaunti yaliyomwagiza kuwafuta kazi Karani wa Kaunti, Dkt Kiambi Atheru Thambura, na Mkuu wa Wafanyakazi wa Kaunti, Harrison Gatobu Nchamba Mbithi kwa kukiuka katiba na sheria nyinginezo.