Habari za Kitaifa

Malala: Walinifurusha UDA kwa kupinga njama ya kumtimua Gachagua

Na KEVIN CHERUIYOT August 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala amejitokeza na kudai alitimuliwa kwa kupinga njama ya kuondolewa afisini kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Malala ambaye amekuwa kimya tangu alipopigwa kalamu Agosti 3, Alhamisi alidai maafisa wakuu wa chama hicho ndio waliongozwa mipango ya kutimuliwa kwake.

“Sikuondolewa kutokana na utepetevu au kushindwa kuendesha shughuli za chama cha UDA. Hatua hiyo ilichochewa na dhana kwamba mimi ni mshirika wa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye alilengwa na hoja ya kumtimua,” Bw Malala akasema jana kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Kulingana na seneta huyo wa zamani wa Kakamega, kichochea kikuu cha kuondolewa kwake kilikuwa “msimamo wangu wa kupinga kuondolewa kwa Gachagua dhana kwamba mimi ndiye nilikuwa kikwazo katika kufanikishwa kwa mipango hiyo.”

Bw Malala alidai kuwa kuondolewa kwa Naibu Rais kulinuiwa kutoa nafasi kwa baadhi ya viongozi wa UDA kutoka Mlima Kenya kujiweka katika nafasi bora kimamlaka kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

“Kuong’olewa mamlakani kwa Bw Gachagua kulihusiana na siasa za 2027 na 2032 katika eneo la Mlima Kenya na kulichochewa na kuendelezwana Bw Cecily Mbarire na Bw Kimani Ichung’wah,” Bw Malala akafichua.

Bi Mbarire, ambaye ni Gavana wa Embu pia ndiye Mwenyekiti wa Kitaifa wa UDA huku Bw Ichung’wah ambaye ni Mbunge wa Kikuyu ndiye Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.

Hata hivyo, Bw Malala alifeli kutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yake.

Alipuuzilia mbali madai kuwa njama ya kumwondoa mamlakani Bw Gachagua ilihusishwa na kuundwa kwa baraza la mawaziri lililoshirikisha viongozi wa chama cha Orange Democratic Alliance (ODM).

Kulingana na Bw Malala njama hiyo ilianzishwa na mahasidi wa kisiasa wa Naibu Rais kutoka ngome yake ya Mlima Kenya.

“Hizi siasa duni zinapasa kushutumiwa kwa sababu zikiachwa kuendelea, zinaweza kutishia uthabiti, umaarufu na uwepo wa chama cha UDA. Rais William Ruto kama kiongozi wa chama, Rigathi Gachagua kama naibu kiongozi wa UDA na mimi tumejizatiti kujenga chama hiki tangu mapema mwaka wa 2022,” Bw Malala akasema.

Katibu huyo Mkuu wa zamani wa UDA pia amemshauri Naibu Rais kuendelea kuwa macho kwani waliopanga njama ya kumwondoa afisini hawajafa roho.

“Natoa ushauri wangu kwa hiari kwa Naibu Rais na Naibu Kiongozi wa chama chetu kwamba asidanganyike kwamba maadui wake wamezima njama ya kumwondoa afisini. Namwambia kwamba wanamapinduzi hao hawajaachana kabisa na njama hizo,” akaeleza.

Huku akiahidi kutoka ushahidi wa kuhimili madai yake dhidi ya Bi Mbarire na Bw Ichung’wah, mwanasiasa huyo anataka wawili hao wang’atuke kwa kupanga njama ya kumwondoa afisini Bw Gachagua.