Habari za Kitaifa

MAONI: Khalwale, Salasya wakomeshe siasa za uhasama wa kikabila

Na CECIL ODONGO April 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SENETA wa Kakamega Bonny Khalwale na mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya wanastahili kukoma kutoa matamshi ambayo lengo lake ni kusababisha uhasama miongoni mwa jamii za Waluhya na Waluo.

Wanasiasa hawa wawili wanaonekana kuanza kutumia suala la miradi na siasa zisizokuwa na mashiko kuzua migawanyiko kati ya jamii hizi mbili ambazo zimeishi kwa amani kwa miaka mingi.

Wikendi, Dkt Khalwale alimshambulia vikali Rais William Ruto akidai kuwa ameshindwa kutimiza miradi mingi ya maendeleo aliyoahidi wakazi wa eneo hilo.

Isitoshe, seneta huyo alizua malalamishi kutokana na ushirikiano wa Kinara wa ODM Raila Odinga na utawala wa Rais Ruto akisema miradi mingi sasa inapelekwa Nyanza badala ya Magharibi.

Akionekana kukerwa, Dkt Khalwale alisema ni kosa kwa Rais kupandisha hadhi Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga (JTRH) jijini Kisumu kabla ya kufanya hivyo kwa ile ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega.

Kiongozi huyo alifasiri kuwa asilimia 30 ya serikali ambayo viongozi wa Magharibi waliafikiana na Rais wakati wa kampeni za kura za 2022, sasa imeenda Nyanza.

Mwanzo, hizi kauli za Dkt Khalwale ni chuki wala sielewei kwa nini Tume ya Kitaifa ya Utangamano na Uwiano (NCIC) bado inasubiri nini kabla ya kumwagiza afike mbele yake.

Ndiyo, yuko sawa kumkaba koo Rais kuhusu miradi ambayo haijatekelezwa lakini hafai kudai kuwa eneo moja limenufaika kwa miradi ambayo jamii nyingine ilistahili kupata.

Kwani watu wa Nyanza si walipa ushuru ndipo Dkt Khalwale aseme hospitali yao haikustahili kupandishwa hadhi kabla ya ile ya Kakamega?

Hizi ni siasa za wivu na kinyongo ambazo zimepitwa na wakati na hazifai kuvumiliwa kamwe.

Hospitali ya JTRH anayoipiga vita seneta huyo imekuwa ikiwahudumia watu kutoka Magharibi, Nyanza na hata wale kutoka Bonde la Ufa ambao hawawezi kufika Nakuru au Eldoret.

Jinsi Rais amekuwa akitembelea Nyanza, ndivyo amekuwa akitembelea pia Magharibi kwa hivyo ni jukumu la viongozi wa kila eneo kupigania kupata miradi waliyoahidiwa.

Kama Raila na viongozi wa Nyanza wamepambana wakapata baadhi ya miradi mbona Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula nao wasipambane eneo lao linufaike ilhali wao pamoja na Dkt Khalwale walimchagua Rais 2022?

Aidha, Bw Salasya naye amekuwa akiendeleza vita vikali dhidi ya ODM na ameanzisha vuguvugu ambalo litawashirikisha vijana.

Vuguvugu hilo linalenga kuzuru Bungoma, Kakamega, Busia na Vihiga kwa lengo la kurai vijana na wakazi wakatae ODM.

Yaani badala ya Bw Salasya kupambania mahangaiko ya wakulima wa Mumias kwenye eneobunge lake, sasa amekubali atumike kuzua mgawanyiko na kujikita kwenye siasa za kijamii.

Wakati wa uchaguzi, kuna vyama vingi ambavyo huwasimamisha wagombeaji Magharibi lakini huwa wanalambishwa sakafu na ODM.

Bw Salasya anastahili kufahamu kuwa ODM hushinda kwa sababu watu hupenda sera zake na pengine ukosefu wa kiongozi imara anayepigania maslahi yao kama Raila.

Siasa za Dkt Khalwale na Bw Salasya kwa kutumia miradi na siasa za chama kutenganisha Nyanza na Magharibi hazitafua dafu na badala yake watafute mbinu nyingine za kuongeza umaarufu wao.

Huwezi kuwatenganisha watu ambao wameoana, wana uhusiano wa kiukoo na wameishi miaka mingi bila kufarakana kutimizia tu maslahi yako ya kisiasa.