Habari za Kitaifa

Masaibu ya wagonjwa wa Saratani dawa muhimu ikikosekana nchini

Na LILYS NJERI March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA zaidi ya mwezi mmoja, wagonjwa wa Saratani nchini wameachwa katika njiapanda, bila kufanyiwa vipimo muhimu kutokana na uhaba mkubwa wa dawa inayohitajika kwa shughuli hiyo.

Kucheleweshwa kwa vipimo hivi kunatoa mwanya hatari kwa seli za Saratani kuongezeka bila kudhibitiwa, jambo ambalo linaweza kuzidisha ugonjwa huo na kuchelewesha matibabu kwa wakati ufaao.

Bi Grace Nduta, mgonjwa wa Saratani ya awamu ya nne, amekuwa akisumbuliwa na kikohozi cha muda mrefu. Daktari wake aliposikia kikohozi hicho, alimtaka afanyiwe vipimo vinavyofahamika kama PET-CT ili kutathmini ikiwa matibabu yake yanahitaji kurekebishwa.

Hata hivyo, alikumbana na changamoto isiyotarajiwa.

“Hakuna vifaa vya kutengeneza dawa inayohitajika kwa kipimo hicho,” aliambiwa katika Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Kenyatta (KUTRRH), moja ya hospitali chache nchini Kenya zinazotoa huduma hiyo.

Kipimo hiki ni muhimu katika kugundua, kupima hatua za ugonjwa, na kufuatilia maendeleo ya matibabu ya Saratani.

Dkt Solomon Mutua, daktari wa Saratani katika Hospitali ya Nairobi West, anaonya kuwa ucheleweshaji huu unaweza kuwa na athari mbaya.

“Kwa wagonjwa wengi wa Saratani, kutambuliwa na ufuatiliaji wa haraka ni muhimu sana. Kucheleweshwa hata kwa wiki chache kunaweza kusababisha ugonjwa kusambaa kwa kasi,” anaeleza.

“Unaweza kutumia kipimo hiki kubaini hatua ya ugonjwa, ikiwa Saratani imesambaa au bado ipo katika eneo moja. Ikiwa Saratani ilikuwa inafanya kazi kwa kasi kabla ya matibabu, basi tunaweza kutumia PET-CT kuona kama imepungua au haipo tena,” alifafanua.

“Mbali na kufuatilia matibabu, kipimo hiki pia kinaweza kusaidia kupanga matibabu, kuhakikisha kuwa matibabu hayo yanakuwa sahihi zaidi. Pia, kinatumika katika ufuatiliaji wa hali ya mgonjwa baada ya matibabu,” alisema.

Nduta si mgonjwa wa pekee aliyeathirika. Kote nchini, wagonjwa wa Saratani wamekuwa wakirudishwa nyumbani kwa sababu ya upungufu wa dawa zinazohitajika kwa vipimo vya PET-CT.

Jumanne , Machi 25, 2025, Hospitali ya Ruai Family, mojawapo ya vituo vinavyotoa huduma hiyo, ilimtumia ujumbe wa maandishi kumjulisha kuwa bado haina huduma hiyo, ikitaja upungufu wa dawa hizo kote nchini.

“Vipimo vimesitishwa hadi taarifa nyingine itakapotolewa,” ilisoma sehemu ya ujumbe huo kutoka hospitali.

Kwa wagonjwa kama Nduta, hali hii ni ya kusikitisha. “Saratani haisubiri, lakini mimi sina chaguo. Ni huzuni na hofu kwa sababu sijui hali yangu ni ipi, na bado ninakohoa. Ninahitaji kulipa Sh55, 000 kupitia Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF) kwa kipimo hiki, lakini nilipokwenda hospitali ya kibinafsi, niliambiwa ni Sh150, 000, pesa ambazo siwezi kumudu,” alisema.

Zaidi ya hayo, aliongeza kuwa amemaliza kiwango cha bima yake ya SHIF na sasa hawezi tena kupata matibabu yaliyo na ruzuku.

Kadiri mgogoro huu unavyoendelea, wagonjwa wa Saratani kama Nduta hawana chaguo lingine ila kusubiri kwa matumaini kuwa hali yao haitazorota zaidi wakati taifa linahangaika kutatua uhaba huu.

Kwa sasa, Saratani ni ugonjwa wa tatu kwa kusababisha vifo nchini Kenya, baada ya magonjwa ya kuambukiza na magonjwa ya moyo.

Takwimu kutoka Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa visa vya Saratani vimeongezeka hadi 42,116 kila mwaka, huku visa vipya 15,566 vikiwa vya wanaume na 26,550 vya wanawake.

Mbali na Saratani, vipimo vya PET-CT pia husaidia kugundua na kufuatilia magonjwa ya ubongo