Mbunge wa Nyeri Mjini apiga abautani baada ya kumpinga Gachagua
MBUNGE wa Nyeri Mjini Duncan Maina Mathenge ambaye mwezi mmoja uliopita, alisimama kwa hoja bungeni akisema alikuwa akimpinga Naibu Rais, Rigathi Gachagua kwa niaba ya wabunge wenzake sita waliochaguliwa katika Kaunti ya Nyeri, amejipata akipiga abautani.
Mbunge huyo alianzisha moja ya mashambulizi makali dhidi ya Naibu Rais kufikia sasa wakati huu wa mazingira magumu ya kisiasa nchini.
“Hotuba yangu hapa pia inawakilisha hisia za Seneta (Kimani Wamatinga) na Mwakilishi wa Kike (Rahab Mukami). Kwa kweli tumeteswa na vitisho na usaliti. Na ni muhimu kama viongozi waliochaguliwa tupewe nafasi ya kutekeleza jukumu ambalo watu wa kawaida wa Nyeri walitupa walipotupigia kura. Haiwezekani kwamba watu wa Nyeri walitupigia kura ili tuweze kumfuata mtu binafsi kote, wakati mtu huyo anaenda kucheza, kunywa Muratina na kula nyama choma. Haiwezekani. Tunataka kuzungumza kutoka hapa ndani ya bunge hili na kufahamisha nchi kwamba heshima ni pande mbili. Hauwezi kutudharau katika maeneo bunge mengine na kutarajia tudumishe heshima ambayo tumekupa kwa miaka miwili iliyopita. Heshima hailazimishwi,” alilipuka na ikabidi atulizwe na Spika Moses Wetang’ula.
Mnamo Julai 31, 2024, Bw Mathenge alikutana na Bw Gachagua wakati wa hafla ya mazishi ya mwanachama wa Baraza la Agikuyu, Bw Charles Kariuki Kabui na akiwa mwenyeji, hangeweza kutoroka kukutana ana kwa ana na Bw Gachagua kabla ya kutangaza kuwa alijutia matamshi yake ya awali.
Alikuwa amepingwa na spika wa Nyeri, Bw James Gichuhi Mwangi aliyemtaka atangaze hadharani ni kwa nini anapigana na Naibu wa Rais na kama alikuwa mmoja wa wanaounda njama ya kumtimua ‘mwana wetu kutoka Rware’( mamlakani)’.
Akijitenga na tetesi za kumtimua Bw Gachagua ofisini, Bw Mathenge alisema hajui ni wapi mikutano ya kupanga mpango huo inafanyika.
“Sitaki kuhusishwa na siasa za ulaghai, unafiki na uongo. Naibu wa Rais anajua kuhusu heshima yangu kubwa kwake. Anafahamu kazi nyingi ambazo tumetekeleza pamoja bungeni. Alinipa nafasi ya kuwa mwenyekiti katika jopokazi la bunge kuhusu mageuzi ya kahawa. Nimejitolea kuhakikisha nitamtuza kwa kupitisha sheria za kusaidia wakulima wetu,” alijitetea.
Alisema: “Pia ningependa kunyenyekeza na kwa dhati naomba msamaha kwa matamshi yangu ya awali. Kulikuwa na kisa cha hivi majuzi ambapo mnamo Mei 19, 2024 Mheshimiwa alikuwa katika hafla ya kanisa katika eneo la Endarasha huko Nyeri na sikufika. Haikuwa makusudi kwani nilikuwa na harambee iliyopangwa awali katika eneo bunge langu na nisingeweza kuwaacha wageni wangu.Kama nilikukosea Bw Naibu Rais kwa kutokuwepo, samahani tena kwa dhati. Iwapo nitakutana na mchakato wa kukutimua, nitasimama kama mtu aliyejiweka hatarini kukutetea. Siku zote nimekuwa nikisisitiza hadharani na faraghani kwamba Bw Gachagua ndiye mfalme wa Mlima Kenya.”
Bw Gachagua aliposimama kuongea, alisikitika kwamba, “kuna watu wachache ambao wamepotoshwa na maadui wa Mlima Kenya na wanatekeleza mipango iliyofadhiliwa ya kugawanya eneo hilo la Mlimani.”