Habari za Kitaifa

Mdomo tamu: Ruto apigia debe azma ya Raila AUC kwa nchi zinazozungumza Kifaransa


RAIS William Ruto ameimarisha kampeni ya Kenya kutwaa uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), huku timu inayopigia debe Raila Odinga sasa ikielekeza juhudi za kupata uungwaji mkono kutoka kwa mataifa ya Afrika yanayozungumza Kifaransa.

Rais Ruto Jumanne alifanya mazungumzo na rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, Amerika, ambapo aliunga mkono Bw Odinga.

Mwenyekiti mwenza wa kampeni ya Bw Odinga, balozi wa zamani wa Kenya nchini Amerika, Elkanah Odembo alisema kwamba ingawa juhudi zao zimeelekezwa kote katika bara la Afrika, wanataka kuanza kuzuru nchi zinazozungumza kifaranza.

Alisema kuwa Bw Odinga katika siku zijazo atazuru mataifa kadhaa yanayozungumza lugha ya Kifaransa kujipigia debe.

“Changamoto ya nchi hizo inachukuliwa kwa uzito mkubwa. Mbali na mikutano huko New York, mgombea wetu amealikwa na nchi kadhaa zinazozungumza lugha ya Kifaransa; Ivory Coast, Togo, Senegal, Algeria, na Morocco,” Bw Odembo aliambia Taifa Leo Jumatano.

Bw Odinga anakabiliana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Youssouf, aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Nje wa Mauritius Anil Kumarsingh Gayan na mwenzake wa zamani wa Madagascar Richard James Randriamandrato.

Mnamo Jumatano akiwa New York, Rais Ruto alikutana na mwenzake wa Angola João Lourenço ambapo walijadili ‘kuimarishwa kwa Umoja wa Afrika.’

Pia alifanya mazungumzo na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini pamoja na Lazarus Chakwera wa Malawi.

Mikutano yake ilijiri baada ya kampeni pembezoni mwa Kongamano la Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC) mjini Beijing, China.

Rais Ruto alikutana na Marais Paul Kagame (Rwanda), Umaro Sissoco Embalo (Guinea-Bissau), Faure Essozimna Gnassingbe (Togo), Mahamat Idriss Deby Itno (Chad), Kanali Assimi Goita (Mali) na Hakainde Hichilema (Zambia), akiwataka kuidhinisha ombi la Bw Odinga.