Habari za Kitaifa

Miradi mitatu ya KDF ya Sh21 bilioni iliyoanzishwa na Kenyatta yakwama

Na EDWIN MUTAI March 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MIRADI mitatu ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) ya thamani ya Sh21.9 bilioni iliyoanzishwa mwisho wa muhula wa mwisho wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta imekwama kutokana na ukosefu wa fedha.

Muda wa kukamilishwa kwa miradi hiyo, iliyoanzishwa kati ya Novemba 2021 na Juni 2022, imepita.

Serikali ya Kenya Kwanza, inayoongozwa na Rais William Ruto, haijatenga mgao wa fedha za kukamilisha miradi hiyo iliyoanzishwa na aliyekuwa bosi na mtangulizi wake.

Dkt Ruto alihudumu kama naibu wa rais chini ya utawala wa serikali ya Bw Kenyatta.

Ripoti ya hivi punde ya ukaguzi wa matumizi ya fedha katika Wizara ya Ulinzi inaonyesha kuwa ni Sh3.16 bilioni pekee zimelipwa kwa wanakandarasi waliopewa zabuni za kutekeleza miradi hiyo mitatu huku Sh18.77 bilioni zikiwa hazijalipwa.

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu, kwenye ripoti ya matumizi ya fedha ya mwaka uliokamilika Juni 2024, anasema wanakandarasi wamesimamisha kazi katika miradi miwili baada ya kukamilisha asilimia 20 pekee, huku kazi za ujenzi zikifikia kiwango cha asilimia 60 katika mradi wa tatu.

“Ukaguzi wa hali ya utekelezaji ripoti katika Wizara inaonyesha kuwa miradi hiyo mitatu, iliyoanzishwa kati ya Novemba 2021 na Juni 2022 na iliyokusudiwa kugharimu Sh21, 946, 793, 240 na iliyofanyiwa malipo ya Sh3, 167, 246, 076 kufikia Juni 30, 2024, imekwama,” Bi Gathungu akaeleza.

“Tarehe ya kukamilishwa kwa miradi hiyo yote imepita,” akaongeza.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa na Utafiti ya Wanajeshi (FRRH) kwa gharama ya Sh18 bilioni eneo la Kabete, Kambi ya Kudumu kwa Kikosi cha 8 Brigade na kikosi cha Mechanized Infantry Battalion (MIB) na Kupanuliwa kwa Barabara ya umbali wa kilomita 4.2.

Ujenzi wa hospitali hiyo, ambayo ingetumiwa na wanajeshi pekee, ulitarajiwa kukamilika mnamo Januari 18, 2025 lakini umekwama baada ya ujenzi wa kima cha asilimia 20 pekee.

Mradi huo ambao kandarasi yake ilitiwa saini Januari 18, 2021 ulizinduliwa na Bw Kenyatta Agosti 31, 2021.

Hospitali ya FRRH ilitarajiwa kutoa huduma maalumu na spesheli kwa maafisa wa asasi za usalama na raia kwa ujumla.

Akiongea alipozindua ujenzi wa hospitali hiyo katika kambi ya kijeshi ya Kabete, Bw Kenyatta alisema mradi huo ni sehemu za juhudi za serikali za kufikia nguzo ya Afya kwa Wote (UHC) katika mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Maendeleo katika serikali yake.

“Hospitali hii ya kiwango cha Level 6 itahudumia maafisa wetu wanaohudumu katika sekta za usalama. Ni siku kubwa kwa nchi yetu na kwa asasi zetu za usalama kwani mradi wa kiwango hiki haujawahi kutekelezwa tangu ujenzi wa Hospitali ya Armed Forces Memorial mapema miaka sabini,” Bw Kenyatta akasema wakati huo.