Habari za Kitaifa

Miradi yachoma mabilioni wagonjwa wakiteseka

Na LINET OWOKO April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MIRADI mikubwa ya afya ya thamani ya mabilioni ya pesa imekwama kote nchini, na kuwaacha wagonjwa mahututi na chaguo chache au ghali kupata matibabu.

Kukwama kwa miradi kama vile Kituo cha Dharura cha Watoto na Usimamizi wa Majeruhi wa Moto katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Kituo cha Saratani cha Kisii, na Kituo cha Ubora cha Taasisi ya Figo Afrika Mashariki kumesababisha msongamano mkubwa hospitalini, vifo vinavyoweza kuzuiliwa, na kuzidisha mgogoro wa afya nchini Kenya, na kuwaacha wagonjwa wengi bila huduma za msingi za matibabu.

Watoto wanaohitaji huduma za haraka za matibabu wanakabiliwa na hatari kwa sababu Kituo cha Dharura cha Watoto na Usimamizi wa Majeruhi wa Moto katika KNH hakijakamilika.

Mradi huo ulipangwa kukamilika mwaka wa 2020 lakini haukuwa umekamilika kufikia Juni 2024, licha ya zaidi ya Sh1.1 bilioni kutumiwa tayari.

Kituo cha majeruhi wa moto kitakuwa na vitanda 82 katika wodi ya kawaida, vitanda 14 vya ICU, na vitanda sita vya wodi ya HDU, huku kituo cha watoto kikiwa na vitanda 82 vya wodi ya kawaida, vitanda 24 vya ICU, na vitanda sita vya huduma maalum.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, kwa mwaka wa kifedha ulioishia Juni 2024 ilibainisha kuwa ucheleweshaji huo umesababisha gharama zisizohitajika za Sh68 milioni – fedha ambazo zingetumika kununua vifaa muhimu vya matibabu, kuajiri madaktari, au kuboresha huduma nyingine za afya.

“Pia, thamani ya kazi iliyofanyika inajumuisha riba ya malipo ya kuchelewesha ya Sh68, 043, 601 ambayo ingeweza kuepukwa. Hii ni kinyume na Kifungu cha 151 (2) (c) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma 2015, ambayo inahitaji taasisi kulipa madeni yake kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba,” alisema mkaguzi mkuu.

Hali ni mbaya vilevile kwa wagonjwa wa Saratani Kisii na maeneo jirani.

Ujenzi wa Kituo cha Saratani cha Kisii, ambacho kingetoa matibabu maalum ya Saratani, umekwama licha ya ufadhili kupatikana miaka tisa iliyopita.

Mradi huo ulipangwa kukamilika mwaka wa 2016, lakini haujakamilika hadi sasa. Ingawa kandarasi ilitolewa Januari 2024, ujenzi haukuwa umeanza kufikia Juni 2024, na kuwaacha wagonjwa bila huduma muhimu za kuokoa maisha.

Ripoti ya mkaguzi mkuu ilibaini kuwa licha ya malipo ya awali ya Sh283 milioni, hakuna kazi yoyote ya ujenzi iliyoanza, huku mamilioni mengine yakitumika kununua vifaa vya matibabu na samani ambazo bado hazijatumika kutokana na ukosefu wa jengo lililokamilika.

Wakati huo huo, wagonjwa wa figo nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla bado wanasubiri kukamilika kwa Kituo cha Ubora cha Taasisi ya Figo Afrika Mashariki cha thamani ya Sh3.7 bilioni, ambacho hakijakamilika miaka sita baada ya tarehe yake ya kukamilika iliyopangwa 2019.

Mradi huo, unaojumuisha jengo la ghorofa tano la shule ya matibabu lenye wodi, maabara, vyumba vya upasuaji, vitengo vya uangalizi maalum, vyumba vya ushauri wa matibabu, na sehemu za maegesho, bado haujakamilika licha ya Sh2.79 bilioni kutumika tayari.

Katika Kaunti ya Kitui, miradi kadhaa ya thamani ya Sh404.58 milioni haijakamilika, baadhi yake ikiwa imekwama tangu 2017, ikiwa ni pamoja na jengo la wodi ya uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kitui (Sh242.78 milioni), jengo la X-ray katika Hospitali ya Kauwi (Sh2.20 milioni), na kiwanda cha gesi ya Oksijeni (Sh14.5 milioni).

Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, miradi mikubwa imesimama, ikiwemo hospitali ya wanawake katika Chuo cha Walimu cha Chesta (Sh37.40 milioni) na jengo la ofisi huko Kapenguria (Sh52.45 milioni).

Kaunti ya Bomet ina miradi ya thamani ya takriban Sh300 milioni ambayo imecheleweshwa au kutelekezwa.

Hii inajumuisha Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto cha Dkt Laboso Memorial (Sh296.93 milioni) na chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Sigor Sub-County (Sh3.99 milioni.