Habari za Kitaifa

Mkewe Kindiki ataka wanafunzi wakumbatie Sayansi

Na CECIL ODONGO March 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKEWE Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Dkt Joyce Kithure amewataka wanafunzi wakumbatie masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati maarufu kama STEM kwa kuwa zinasaidia kusuluhisha matatizo ibuka katika jamii.

Dkt Joyce (pichani) amesema masomo hayo ndiyo msingi wa uvumbuzi ambao utasaidia Kenya kupambana na changamoto zinazozingira nchi kiuchumi, kimazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Alikuwa akiongea katika Chuo Kikuu cha Daystar wakati wa kuadhimisha siku ya masomo ya Sayansi na Hisabati. Hasa alisema kozi hizo zitawapa vijana nafasi kubwa ya kujiajiri ikizingatiwa nafasi za ajira serikalini nazo zimeadimika.

“Hatusherehekei Sayansi tu bali pia tunaamsha hamu ya wavumbuzi siku zijazo hasa wale ambao watajihusisha na taaluma zinazofungamana na masomo haya,” akasema.

Dkt Joyce ni msomi ambaye anafundisha Kemia katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Alitaja hatua zilizopigwa katika kutumia Hisabati na Teknolojia kuvumbua mtandao wa malipo ya kidijitali ya Mpesa na mashine zinazotumia upepo kuzalisha kawi mashambani.

Aliwataka wavumbuzi chipukizi kusaka suluhu kwa changamoto za nchi ili kuimarisha hali ya maisha na mapato akisema masomo ya sayansi ndiyo kitega uchumi wa kwa sasa.

“Dunia inahitaji talanta yenu, mawazo na ari ya kuvumbua. Nyinyi ndiyo mtaamua mkondo ambao taifa litachukua,” akasema.

Wakati wa hafla hiyo alizindua mradi ambao unaangazia mazingira na jamii. Mradi huo unalenga kuhakikisha kuna maji safi, uchafuzi wa mazingira unapunguzwa, kuna kawi safi na pia changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi zinatatuliwa.