Habari za Kitaifa

Mlaghai wa KCSE kupitia Telegram akamatwa; waziri akemea watu wanaopaka tope mtihani

Na WYCLIFFE NYABERI November 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Elimu Julius Ogamba anataka washukiwa wanaolaghai Wakenya kuwa watawauzia karatasi za mtihani unaoendelea wa KCSE kupitia mtandao wa Telegram kuchukuliwa hatua za haraka za kuadhibiwa.

Haya yanajiri baada ya kukamatwa kwa Bw Stephen Nyang’au Mbeche, msimamizi anayedaiwa amekuwa akiwalaghai Wakenya kwa kujifanya kuwa ana karatasi za mtihani huo unaoendelea.

Tapeli huyo mwenye ujuzi wa teknolojia, amekuwa akiwalaghai Wakenya pesa kwa kutumia kundi moja la Telegram, liitwalo “KCSE 2024 Leakage Group”

Maafisa wa upelelezi wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC), walimkamata Bw Mbeche katika eneo moja lililoko Masaba Kaskazini, Kaunti ya Nyamira.

Makachero hao walitwaa kipakatalishi kimoja, simu ya mkononi na vifaa vingine ambavyo wanaamini amekuwa akitumia kwa ulaghai huo.

“Mashtaka dhidi yake yanaandaliwa na atafikishwa mahakamani kwa wakati, kikosi cha makachero wetu kinaendelea kuwasaka watu wengine waliohusika katika ulaghai huo,” polisi walisema.

Akizungumza Jumatatu, Novemba 11, 2024, aliposimamia usambazaji wa karatasi za mitihani eneo la Lang’ata, Bw Ogamba alisema atazidi kuunga mkono wasimamizi wa mtihani huo ili kufanya kazi yao kikamilifu.

Aliongeza kuwa wameiomba Mahakama kuharakisha kesi zinazohusu udanganyifu wa mitihani na kutoa adhabu kali kwa wale watakaobainika kuwa na hatia.

“Tumeomba Idara ya Mahakama itusaidie kuhakikisha kuwa kushtakiwa kwao ni kwa haraka ili watu wakabiliwe na sheria. Hapo awali, kushtakiwa kwao kumechukua muda mrefu hadi wanasahau kuwa udanganyifu wa mitihani ni hatia na kwa hivyo wanaendelea kurudia,” Bw Ogamba alisema.

Aliwasifu wasimamizi wa mtihani huo kwa kujitolea kwao ili kuhakikisha watahiniwa wanafanya mtihani wao inavyohitajika.

“Mnafanya kazi kwa bidii sana. Mnaamka mapema. Mko pale mnahangaika halafu mtu mmoja au wawili waliofanya mtihani huu biashara wanatupa jina baya. Tunataka kusafisha sekta hii, tunataka kufanya mambo sahihi. Tuna wajibu kwa nchi yetu,” Bw Ogamba alisema.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo wiki jana, ulibaini kuwa matapeli hao walikuwa wakiuza karatasi hizo kati ya Sh2,500 na Sh18,000 kulingana na karatasi mtu alihitaji.